Jumanne Sagini, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (OWM - TAMISEMI) |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KATIKA hali inayoonesha kwamba ni utendaji mbovu katika
kuongoza sekta ya umma na kuendelea kupandikiza chuki miongoni mwa jamii,
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani hapa, Hussein
Ngaga ameendelea kulalamikiwa na baadhi ya Madiwani wake kwamba amekuwa
akisambaza pesa (Rushwa) kwa lengo la kushinikiza madiwani hao wajenge hoja ya
kumkataa Afisa elimu msingi wa wilaya hiyo, Mathias Mkali. Mtandao huu
umeelezwa.
Kadhalika inadaiwa pia Gaudence Kayombo, Mbunge wa jimbo la
Mbinga naye amekuwa akishiriki kwa namna moja au nyingine kushawishi baadhi ya
Madiwani wamkatae afisa elimu huyo, kwenye kikao cha baraza la madiwani hao
ambacho kitaketi mwishoni mwa mwezi huu.
Siri hiyo imevuja baada ya wengi wao wakishangaa na wengine
kuchukizwa na kitendo hicho wakihoji kwa nini wanafanya hivyo, na kuwataka
waachane na tabia hiyo ambayo huenda baadaye ikawageuka wao wenyewe na kuwaweka
mahali pabaya.
Mwandishi wa habari hizi ameelezwa na vyanzo vyetu mbalimbali
kuwa, kwa nyakati tofauti vikao vimekuwa vikifanyika ofisini kwa mkurugenzi
huyo na hata nyumbani kwake, kupanga mikakati ya kuhakikisha jambo hilo
linafanikiwa kwa njia yoyote ile.
Mwenyekiti wa Kamati ya elimu afya na maji katika baraza la
madiwani la halmashauri ya wilaya ya Mbinga, James Yaparama amekiri kupokea
taarifa hizo kutoka kwa baadhi ya madiwani wenzake na kusema tabia hiyo
wanayoifanya sio nzuri huku akidai kuwa fedha wanazotumia kuwagawia madiwani hao,
huenda zikawa ni kodi za wanambinga ambazo ilibidi zikafanye shughuli nyingine
za maendeleo ya wananchi.
“Huyu Mkurugenzi sisi tunamshangaa sana, tokea muda mrefu
wakati anaanzisha ugomvi huu na kufikia kumsimamisha kazi mwenzake (Afisa elimu
msingi) bila kufuata taratibu, mara nyingi amekuwa akitumia nguvu kubwa ya pesa
kutaka tu kumkandamiza mwenzake wakati hana kosa lolote na hivi anavyofanya
mwisho wake nini”?, alihoji James.
Gaudence Kayombo alipoulizwa juu madai hayo alisema, “huna
haja ya kuniuliza kwa hayo unayosema, wewe tabia yangu unaifahamu, na kuishia
kukata simu”.
Kadhalika kwa nyakati tofauti mwandishi wetu amezungumza na
baadhi ya wadau mbalimbali wa elimu wilayani Mbinga, wamesema kuwa Taasisi ya
kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani humo licha nayo kupelekewa
malalamiko mengi juu ya mwenendo mbaya wa mambo mbalimbali ya utumishi wa umma,
yanayoendelea kufanywa katika halmashauri hiyo hakuna hatua zilizochukuliwa na
kuzaa matunda hadi sasa.
Walisema katika wilaya ya Mbinga taasisi hiyo ni sawa kama
imeenda likizo, hivyo ni vyema serikali ikachukua hatua nyingine ya
kushughulikia matatizo ya wananchi wilayani humo, lakini sio kwa hali hiyo
ambayo inaendelea kuumiza wananchi.
Hivi karibuni waandishi wa habari walipozungumza na Kamanda
wa TAKUKURU wa wilaya hiyo, Ditram Mhoma ili aweze kuzungumzia juu ya madai
hayo ya wananchi kwamba taasisi hiyo imeenda likizo haishughulikii malalamiko
yao ipasavyo, alisema sio kweli wao wanafanya kazi hawana mchezo na mtu.
Kwa upande wa watu kumlalamikia Mkurugenzi mtendaji wa Mbinga
Bw. Ngaga, kamanda huyo wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa alikiri
kupokea malalamiko hayo na kuonekana akimtetea akisema ni kiongozi mzuri,
ambaye hana matatizo katika kuwaongoza wananchi.
“Kaka naomba niwaelezeni, huyu Mkurugenzi wa Mbinga ni mzuri
sana tunafanya naye kazi vizuri na anatupatia ushirikiano wa kutosha pale
tunapofanya kazi zetu”, alisema Mhoma.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga
Hussein Ngaga alipotafutwa ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya malalamiko hayo,
hakuweza kupatikana na simu yake ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa,
na imekuwa ni tabia yake ya kutopokea simu na kukataa kuhojiwa na waandishi wa
habari.
No comments:
Post a Comment