Na Gideon Mwakanosya,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linawasaka watu
wanne wanaodhaniwa kuwa ni majambazi ambao wanadaiwa kuwapiga risasi watu
wawili, katika matukio tofauti likiwemo la mwanamke ambaye ni mhudumu wa
baa kujeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi mgongoni, kisha kunyanganywa simu
ya mkononi yenye thamani ya shilingi 35,000 na kutokomea nayo kusiko
julikana.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela alisema kuwa
matukio yote mawili yametokea majira ya saa za usiku huko katika maeneo
ya Mabatini kata ya Misufini na Mfaranyaki mjini songea.
Kamanda Msikhela alisema kuwa tukio la kwanza
lilitokea majira ya saa mbili usiku huko katika mtaa wa mabatini kwenye
eneo la kando kando ya ukuta wa msikiti wa , uliopo kata ya Misufini ambapo
Fatuma Hamisi (29) ambaye ni mhudumu wa baa ya Olympic iliyopo mjini hapa, wakati
akielekea kazini kwake ghafla alifuatwa na kijana mmoja mwembamba
aliyevalia kofia aina ya mzura ambaye hakufahamika kwa jina, na kumuamuru
Fatuma asimame.
Alisema kuwa wakati Fatuma anamsimamisha, kijana huyo aliamua
kutoa silaha ambayo baadaye alifyatua risasi moja hewani huku akimtaka
amkabidhi simu aliyokuwa nayo mkoni lakini, msichana huyo aliendelea kugoma
kumpatia simu kisha alimfyatulia risasi nyingine mgongoni na kumnyanganya simu
aina ya ITEL yenye thamani ya shilingi 35,000.
Kwa sasa hivi Fatuma amelazwa katika hospitali ya mkoa Songea,
kwa matibabu zaidi na hali yake bado ni mbaya kwani madaktari wanaendelea
kumfanyia uchunguzi zaidi.
Kamanda Msikhela alieleza kuwa hivi sasa jeshi la polisi
linaendelea kumsaka mtuhumiwa wa tukio hilo, ambalo limeleta hofu kubwa kwa
wakazi wa eneo hilo.
Alilitaja tukio lingine kuwa lilitokea January 8 mwaka huu
majira ya saa tisa usiku kwenye maeneo ya mtaa wa gereji ya kisiwa kata ya
Mfaranyaki Manispaa ya Songea, ambako Mussa Mchopa (50) ambaye ni Meneja
wa baa ya Sovi mjini humo akiwa amelala nyumbani kwake alivamiwa na kundi
la watu wanne wasiofahamika ambao kabla ya uvamizi huo walivunja mlango na
kuingia ndani ya nyumba hiyo.
Watu hao wanaodaiwa kuwa ni majambazi wakiwa ndani ya
nyumba hiyo walimvamia Mchopa na wakati wa kurupushani hizo, Mchopa alipambana
na watu hao huku tayari wakiwa wamemjeruhi kwa kumpiga risasi eneo la kichwani
na baadaye walikimbia bila kuchukua kitu chochote.
Wakati wanakimbia walidondosha
bunduki aina ya CHINESE PISTOL yenye namba za usajili 2000911 ambayo
ilikuwa na risasi saba, huku ganda moja la risasi limekutwa kwenye eneo la
tukio na polisi inaendelea kufanya uchunguzi ili kuwapata watuhumiwa wa matukio
yote mawili.
Alieleza majeruhi Mchopa ametibiwa katika hospitali ya
mkoa Songea na ameruhusiwa na hali yake inaendelea vizuri.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa Songea Dokta Benedict
Ngaiza alisema kuwa usiku wa kuamkia jana, majeruhi wawili wamepokelewa ambao
wanadaiwa kuwa walipigwa risasi katika matukio mawili tofauti ambapo alidai
kuwa Fatuma ambaye amelazwa katika wodi namba mbili ya majeruhi hali yake
bado si nzuri, na uchunguzi unaendelea kufanywa kwani alipigwa risasi mgongoni
ambako kuna jeraha kubwa na Mchopa aliletwa hospitalini hapo akiwa na jeraha
kichwani ambalo inadaiwa alipigwa risasi na watu wasiofahamika lakini ameruhusiwa
na hali yake inaendelea vizuri.
No comments:
Post a Comment