Nassib Abdul, maarufu Diamond Platinum |
Na Mwandishi wetu,
Songea.
MKOA wa Ruvuma, umepata heshima kubwa ya kuandaa sherehe za
kutimiza miaka 38 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitaifa mwaka huu.
Mbunge wa Songea Mjini Dokta Emmanuel Nchimbi ameanza
kuratibu sherehe hizo ambazo zitafanyika mkoani humo, na mgeni rasmi
anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Rais Jakaya Kikwete.
Dokta Nchimbi alisema hayo alipokuwa akizungumza na vyombo
mbalimbali vya habari mjini hapa, ambapo kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni; Umoja
ni Ushindi, Katiba yetu nchi yetu.
Mbunge huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi,
alisema kila kitu kimekamilika juu ya maandalizi ya sherehe hizo ambazo
zitafanyika Februari Mosi mwaka huu, badala ya Februari tano kama
ilivyozoeleka.
“Februari tano ni siku ya kazi, sasa tusiharibu utaratibu wa
watu, tumeona tuiweke tarehe hii katika kuadhimisha sherehe hizi za chama cha
mapinduzi” alisema.
Alisema mabadiliko hayo yanalenga kuwapa fursa wananchi wengi
ili waweze kushiriki, siku hiyo ambayo itakuwa siku ya Jumapili.
Maandalizi ya vijana wa halaiki, uwanja na vikundi mbalimbali
vya ngoma yanaendelea, vijana wa bendi kutoka Zanzibar wameshawasili na
wanaendelea na mazoezi, bendi yetu ya Tanzania One Theatre (TOT) nayo
itatumbuiza.
Kadhalika watakuwapo wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi
kipya wakiongozwa na Nassib Abdul maarufu kama Diamond Platinum.
Naye Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho alisema
chama hicho kimeendelea kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo kama ilani
inavyoelekeza kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.
“Tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu, afya,
maji na miundombinu huku barabara nyingi zimejengwa kwa kiwango cha lami
ikilinganishwa na miaka iliyopita,” alisema Mwisho.
No comments:
Post a Comment