Tuesday, December 30, 2014

MKURUGENZI MTENDAJI MBINGA AMDANGANYA RAIS KIKWETE, ADAIWA KUPANGIA MATUMIZI FEDHA ZA WAKULIMA WA KAHAWA KINYUME NA TARATIBU ZA USHIRIKA

Rais Jakaya Kikwete.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MALALAMIKO yaliyotolewa juu ya shilingi bilioni 2 ambazo baadhi ya vyama vya ushirika (AMCOS) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, vilikopeshwa na shirika la hifadhi ya jamii (NSSF) na kuleta gumzo kuwa Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Hussein Ngaga, hakuzipeleka kwenye vyama hivyo badala yake alidaiwa kuziingiza kwenye akaunti ya halmashauri ya wilaya hiyo tumebaini kwamba, fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti husika za vyama hivyo huku akitoa masharti kwa uongozi wa AMCOS hizo kuwa, hawana ruhusa ya kuzifanyia matumizi ya kukopeshana mpaka idhini itoke kwake.

Aidha mkurugenzi huyo analalamikiwa kuwa viongozi hao wa vyama vya ushirika, alikuwa akiwapangia matumizi ya fedha hizo baada ya yeye kujiridhisha kwanza wameandaa mpango kazi wa mahesabu husika na kiasi cha kahawa walichonacho ambayo itaingizwa kiwandani, ndipo alikuwa akiwaruhusu kwenda kutoa fedha benki huku akihakikisha hundi walizoandika zina kiwango halisi anachokifahamu.

Na wakati mwingine analalamikiwa kuwa, alikuwa hawapatii fedha kwa kiwango walichoomba katika mahesabu hayo ambayo walikuwa wakimpelekea ofisini kwake kwa ajili ya kuyakagua na kujiridhisha, badala yake alikuwa anapunguza kwa kiwango anachokitaka yeye.

Tumebaini pia baada ya mauzo ya kahawa kufanyika mnadani Moshi, hivi sasa mkurugenzi Ngaga amekuwa akikwepa kutoa Fomu ya mauzo ya kahawa kwa dola (Account Sale) kwa wanaushirika hao, licha ya wao kumfuata mara kwa mara wakimtaka awapatie.

Katika fomu hiyo huonyesha kahawa ambazo zimeuzwa kwa dola na ubadilishaji wa fedha za mauzo ya kahawa kutoka kiwango cha dola kuwa shilingi, hivyo inadaiwa huenda zimeuzwa kwa bei ya juu huku wanaAMCOS hao wakimlalamikia kuwalipa bei ndogo, ndio maana hataki kutoa fomu hizo na kuweka mchakato huo wa mauzo kuwa bayana ili wakulima waweze kufahamu juu ya mauzo ya kahawa yao ulivyofanyika.

Hali hiyo imeelezwa na wakulima hao kuwa huenda anaficha ukweli halisi usiweze kujulikana juu ya mwenendo mzima wa mauzo ya kahawa yao ulivyofanyika huko mnadani kwa kila mkulima (vikundi).


Tendo hili lililofanywa na mkurugenzi huyo ambalo analalamikiwa kushirikiana na viongozi wachache wa vyama hivyo vya ushirika ambao yeye anadaiwa kula nao na kusuka mpango huo wa kutotoa fomu hiyo ya mauzo, linafananishwa kama wizi na kwamba baadhi ya wakulima walioshiriki katika mauzo ya kahawa zao walisema wanampango wa kwenda kumuona Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu ili wakatoe malalamiko yao juu ya mwenendo huo wanaofanyiwa.

Ngaga analalamikiwa kuwa AMCOS hizo tangu mauzo ya kahawa yao ufanyike huko mnadani Moshi, hawajashirikishwa kikamilifu badala yake halmashauri na watu wake wachache ambao majina yao tunayo, aliwateua kufanya ufuatiliaji kuanzia kahawa inaingizwa kiwandani kwa ajili ya kukobolewa mpaka inasafirishwa kwenda mnadani, ndio wanatajwa kuhusika na mchakato mzima wa mauzo ya kahawa hiyo ya mkulima huku wenye kahawa yao wakibaki kushikwa na kigugumizi, wakihoji kulikuwa na umuhimu gani wa kukopeshwa fedha hizo na NSSF kama halmashauri inaingia katika kufanya biashara hiyo?

Imeelezwa kuwa kitendo kilichofanywa na mkurugenzi huyo ni ukiukwaji wa sheria na taratibu za ushirika, hivyo alitakiwa fedha hizo azifikishe kwanza kwenye ushirika kwa kufuata mgawo husika na sio yeye kuzipangia matumizi na kwa kufanya hivyo, amemdanganya Rais Jakaya Kikwete kwa kauli yake aliyoitoa hivi karibuni mbele yake kwamba fedha hizo watakabidhiwa walengwa wa vyama vya ushirika.

Rais Kikwete mnamo Julai 19 mwaka huu, alikabidhi hundi kwa viongozi wa vyama vya ushirika ambavyo vilikopeshwa fedha hizo alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo, kwa vyama vinne ambavyo vilipewa mkopo huo na shirika hilo.

Vyama vinne vya ushirika ambavyo vilipatiwa mkopo huo ni Mahilo, Ngaka, Ngima na Pilikano ambapo hujishughulisha na uzalishaji wa zao la kahawa wilayani humo, na kila kimoja kilipewa shilingi milioni 500 ili wakulima yaani wanakikundi waliomo ndani ya ushirika huo waweze kukopeshana, lakini mkurugenzi Ngaga alitengeneza utaratibu anaoujua yeye na kuvipatia fedha kidogo kidogo kulingana na kiasi cha kahawa, inayoingizwa kiwandani kwa ajili ya kukobolewa ndio maana leo analalamikiwa.

Baadhi ya watumishi wa halmashauri ya wilaya hiyo (majina tunayo) walionekana muda mwingi wakitumia magari ya halmashauri kutia mafuta ambayo ilibidi yakafanye shughuli nyingine za maendeleo ya wananchi vijijini, wakilipana posho na kufanya ufuatiliaji kuhakikisha kwamba vikundi vinapeleka kahawa kiwandani ndipo vinakopeshwa fedha, jambo ambalo watu wengi walikuwa wakihoji inakuwaje halmashauri inaingia katika biashara ya kahawa?

Wakulima wa vyama hivyo vya ushirika walipozungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, walidai kuwa huenda Mkurugenzi huyo alifanya hivyo akiwa na makusudi yake binafsi, ili fedha hizo aweze kunufaika nazo kwa namna moja au nyingine na sio mkulima kama shirika la NSSF lilivyo lenga.

Baadhi ya wakulima ambao walikopeshwa fedha hizo walisikitishwa na kitendo hicho, wakieleza kuwa wao wanachoelewa ni kwamba fedha hizo baada ya kuingizwa kwenye akaunti za vyama vyao vya ushirika ilibidi aache kuingilia taratibu za ushirika,  na wanachama kupitia viongozi wao wajipangie taratibu za kukopeshana kulingana na sheria za ushirika zinavyosema.

Waliongeza kuwa licha ya NSSF kukopesha kwa riba nafuu ya asilimia 9 bado mkulima huyo kwa malipo ya kwanza alilipwa shilingi 2,500 na ya mwisho shilingi 2,000 huku ndani ya bei hizo wakilazimika kulipa gharama zote za usafiri na kodi mbalimbali huku wakibakiwa na kiasi kidogo cha fedha, jambo ambalo wanamashaka nalo wakidai kwamba wanaibiwa, kwani makampuni binafsi yamekuwa yakinunua kahawa kwa mkulima shilingi 4,800 hadi 5,000 na yamekuwa yakilipa riba kubwa benki ya asilimia 24 na gharama za usafiri yakijitegemea yenyewe.

Wengi wao wamekuwa wakihoji inakuwaje mkopo huo wa riba nafuu, uliotolewa na shirika hilo, mkulima alipwe fedha kidogo tofauti na bei inayolipwa na makampuni binafsi kwa wakulima, ambapo hukopa fedha benki kwa riba kubwa? 

Hata hivyo jitihada ya kumpata Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Bw. Ngaga ofisini kwake ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya malalamiko haya hazikufanikiwa na simu yake ya kiganjani ilikuwa haipatikani.


No comments: