Na
Steven Augustino,
Tunduru.
UCHAGUZI
wa Serikali za Mitaa ambao umefanyika hivi karibuni Disemba 14 mwaka huu, umeacha
makovu wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma kwa baadhi ya viongozi na wakereketwa wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kuchomewa moto nyumba zao na watu
wasiojulikana, na kusababisha hasara kubwa ya kuunguliwa mali zilizomo ndani ya
nyumba hizo pamoja na kukosa makazi.
Taarifa
za tukio hilo zinaeleza kuwa Diwani wa kata ya Ngapa Rashid Issaya na
mwanachama wake Hassan Liugu nyumba zao zilichomwa moto, baada ya kuzuka malumbano
ya kisiasa na kuwasababishia hasara kubwa ya kuungua nyumba zao pamoja na mali
zilizokuwemo ndani yake.
Sambamba
na tukio hilo, mfuasi mmoja wa Chama Cha Wananchi (CUF) Yashua Kawisa (21)
ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mbesa wilayani humo, naye amejeruhiwa vibaya kwa
kukatwa mapanga, wakati akiwa katika kampeni za uchaguzi huo.
Taarifa
za tukio hilo zinaeleza kuwa majeruhi huyo alikatwa panga, katika paji la uso na
kukimbizwa katika hospitali ya Misheni Mbesa kwa matibabu zaidi.
Akizungumzia
mkasa huo ofisa mtendaji wa kata ya Mbesa Rasso Kundete, alisema kuwa majeruhi
Kawisa alijeruhiwa na mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa serikali kitongoji cha
Luwawa, anayefahamika kwa jina la Alex Mchopa wakati wakiwa katika mchakato wa
kampeni za mwisho usiku wa kuamkia Disemba 14 mwaka huu.
Naye
Mtendaji wa kata ya Ngapa, Zuberi Ngoma alisema kuwa chanzo cha matukio hayo
kilisababishwa na vijana na wafuasi wa Chama Cha Wananchi (CUF) wilayani
Tunduru, kukataa kupokea matokeo ya uchaguzi huo baada ya kuonekana kuwa
mgombea wa CCM alikuwa ameibuka na ushindi baada ya kupata kura 350 huku wao
wakiwa na kura 290.
Kamanda
wa Polisi mkoani Ruvuma, Mihayo Msikhela amethibitisha kuwepo kwa matukio hayo
na kueleza kuwa Polisi wanaendelea kufanya uchunguzi ili kuweza kuwapata
watuhumiwa na chanzo cha matukio hayo.
Msikhela
aliendelea kufafanua kuwa nyumba ya diwani Isaya ilichomwa moto mchana wa
Desember 14 mwaka huu majira ya saa 8:30 mchana, na kwamba tukio la kuchomwa
kwa nyumba ya Liugu lilitokea majira ya saa 2:00 usiku siku ulipofanyika
uchaguzi huo.
Kuhusu
tukio la majeruhi Alex Mchopa ambaye amelazwa katika hospitali ya Misheni Mbesa,
alisema polisi wanaendelea kumtafuta mtuhumiwa kwa kushirikiana na askari wan
chi jirani ya Msumbiji, ambako inadaiwa kuwa mtuhumiwa amekimbilia huko.
No comments:
Post a Comment