Saturday, December 27, 2014

UVCCM RUVUMA YAITAKA JAMII KUFARIJI WAGONJWA



Steven Augustino na Abbas Mlanya,
Tunduru.

UMOJA wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani Ruvuma, umewataka wadau mbalimbali kujenga tabia ya kuwatembelea wagonjwa ambao wamelazwa hospitalini, kwa lengo la kuwafariji na kuwapatia zawadi hasa katika kipindi cha sikukuu za kitaifa.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa umoja huo mkoani hapa, Alex Nchimbi wakati alipowatembelea wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya wilaya ya Tunduru.

Aidha Nchimbi ambaye aliongozana na viongozi wenzake wa chama cha mapinduzi wilayani humo, wakiwemo wakiwemo katibu wa CCM wilaya Mohammed Lawa, Abdakah Zubery Mmala (Mwenyekiti wa UVCCM wilaya), Jumma Khatibu (Katibu UVCCM wilaya) wakiwemo pia makada na wakereketwa wa chama hicho.


Ujumbe huo alioongozana nao ulibeba zawadi mbalimbali na kuwapatia wagonjwa, ambapo  waligawa mafuta ya kupaka, sabuni, miswaki na dawa zake vyote vikiwa na thamani ya shilingi 400,000.   

Nchimbi alipohojiwa na waandishi wetu alisema, haileti maana kwa kiongozi aliyechaguliwa na wananchi kukaa ofisini tu wananchi wake wakiwa wanaugua au kusumbuliwa na matatizo mbalimbali, bila kutoa msaada au kuwafariji na pasipo kufanya hivyo ni dhambi.

“Utaratibu huu wa kutembelea wagonjwa na kuwafariji, sisi chama cha mapinduzi maeneo mengi hapa nchini tumekuwa tukitekeleza hili”, alisema Nchimbi na kuwataka vyama vingine kuiga mfano huo.

Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya wilaya ya Tunduru, Kaimu mganga mkuu wa wilaya hiyo Aureus Mhagama pamoja na mambo mengine aliwapongeza viongozi hao kwa uamuzi walioufanya wa kuja kuwaona wagonjwa huku akiwataka waendelee kuwa na moyo wa namna hiyo. 

Katika usiku wa kuamkia sikukuu ya Krismasi hospitali ya wilaya hiyo ilipokea wagonjwa 10 akina mama wajawazito, ambapo kati yao wagonjwa 6 walijifungua salama, wanne bado walikuwa hawajajifungua huku idadi ya watoto hao ikiwa inafanana yaani wanaume 3 na wanawake 3.

No comments: