Wednesday, December 10, 2014

ACHENI TUME IFANYE KAZI ZAKE KWA UHURU BILA KUINGILIWA

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HATIMAYE serikali, imechukua hatua ya kuunda tume na kuileta katika halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu juu ya tuhuma anazotuhumiwa Afisa elimu msingi wa wilaya hiyo Mathias Mkali.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Hussein Ngaga ndiye aliyeibua hoja kadhaa za kumtuhumu afisa elimu wake, na kufikia hatua ya kumsimamisha kazi kwa muda, hadi tume hii leo inaripoti hapa Mbinga kwa ajili ya kuja kuchunguza tuhuma hizo kwa lengo la kupata ukweli na kutoa ushauri nini kifanyike.

Kwa ujumla tunapenda kuipongeza serikali kwa jitihada hizi ilizozifanya, na kwamba tunashauri tu kwa kuiomba tume hiyo isimame kidete katika kutenda haki kwa pande zote mbili yaani aliyetuhumu na mtuhumiwa, ili wananchi siku ya mwisho tuweze kutambua ukweli wa jambo hili upo wapi, ambapo kila kukicha limekuwa likikera na kuleta mgogoro ambao umedumu kwa muda mrefu sasa.


Mgogoro huu umeifanya hata wilaya hii, kufikia hatua ya viongozi kutoelewana na kutupiana vijembe ambavyo havina tija katika jamii, badala ya kukaa na kujenga misingi ya kufanya kazi, watu wanaishia kila kukicha kulumbana pasipo sababu za msingi.

Wananchi wa Mbinga wanachohitaji kuona maendeleo yanafanyika, na sio watu kulumbana kila kukicha. Hakika hili la uundaji wa tume na kuja kuchunguza jambo hili tuna imani haki itatendeka.

Hatutaki kusikia au kuona tena kuna malalamiko kwamba tume haijatenda haki au kuna mianya ya kupenyeza rushwa, wakati Madiwani kwa muda mrefu wamekuwa wakilia juu ya jambo hili na kutaka tume, juu ya mambo mengi aliyokuwa ametuhumiwa afisa elimu huyo wakisema kuwa sio ya kweli bali ni mambo ambayo yalikwisha pitishwa kwenye vikao husika kabla hata mkurugenzi huyu hajahamia hapa Mbinga kuja kufanya kazi.

Nakumbuka wakati wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Shaibu Nnunduma ndiye aliyepitisha na baraza lake la madiwani mambo mengi (nakala tunazo) ambayo leo yamegeuzwa kuwa tuhuma, hivyo nashauri itakuwa busara kuona hata mkurugenzi huyo ambaye sasa yupo wilaya ya Nyasa hapa mkoani Ruvuma, naye anaitwa na kuhojiwa na tume hii ili tuweze kupata ukweli na undani wa jambo hili, ambalo linaleta mgogoro ambao unaendelea kufukuta na kutishia kukua kwa maendeleo katika sekta hii muhimu ya elimu.

Licha ya kuhojiwa mkurugenzi huyu pia baadhi ya madiwani nao waitwe, walimu, waratibu elimu kata na hata wadau wengine muhimu wa elimu, nao wahojiwe tuweze kupata ukweli zaidi wa jambo hili.

Nashauri pia tume ipewe uhuru wa kufanya kazi yake, sio ifikie mahali tusikie kwamba inaingiliwa na kiongozi fulani, eti kwa sababu ya matakwa yake binafsi, kwa kweli tukifanya hivi hatutaitendea haki jamii hii ya wanambinga.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Mbinga, tunakutaka tulia acha tume ifanye kazi zake hatuhitaji leo kusikia linaibuka hili mara lile, wewe ni kiongozi ambaye serikali ilikuamini na kukupatia mikoba ya kuwaongoza wanambinga, hivyo unachopaswa ni kusimama katika misingi ya haki na sio vinginevyo.

Vurugu za kupigiana kelele na kufokeana kama watoto wadogo kwa viongozi wenzako haya mambo yalikwisha pitwa na wakati, acha tume ifanye kazi zake ili mwisho wa siku tupate kujua mkweli ni nani? Tumesikia kwamba tayari inadaiwa kuna mbinu chafu zimeanza kutengenezwa ili kupenyeza mambo unayoyataka wewe, tunashauri huu sio utawala bora hebu acha tume ifanye kazi yake, sisi wanaharakati tutaendelea kusema ukweli daima kila kukicha juu ya jambo hili kamwe hatutanyamaza kimya pale tutakapobaini uchafu unatendeka.

Sisi wananchi wa Mbinga tunaimani kwamba haki ndio msingi wa mambo yote duniani, hivyo tunasema hatutaki kuona tume inaingiliwa tuiache ifanye kazi zake kwa misingi na taratibu husika zilizopo, ili baadaye mwisho wa siku iweze kujenga misingi yenye kuleta usawa bila uonevu.

Mwandishi wa makala haya ya uchambuzi anapatikana kwa simu namba 0762578960 au barua pepe nyandindi2006@yahoo.com



No comments: