Na Steven Augustino,
Tunduru.
WAFANYABIASHARA na walipa kodi wanaotakiwa kutumia
mashine za kielektroniki (EFD'S) wilayani Tunduru mkoani hapa, wameiomba serikali
inunue mashine hizo na kuzigawa bure kwa wafayabiashara hao, ili ziweze kusaidia
serikali kukusanya kodi husika.
Ombi hilo limetolewa na wafanyabiashara hao wakati walipokuwa
wakizungumza na maafisa waandamizi wanaosimamia ukusanyaji wa kodi, katika mkutano
uliofanyika kwenye Ukumbi wa New generation uliopo mjini hapa.
Mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Kazembe Said
ndiye aliyeanza kufanya uchokonozi wa kupenyeza ombi hilo, na kuongeza kuwa
pamoja na mambo mengine wao hawapingani na taratibu za ulipaji wa kodi, isipokuwa
kinacho wakwaza ni kutokuwa na mitaji ya kutosheleza kununua mashine hizo.
Wakati wafanyabiashara hao wakionekana kuunga mkono
ombi hilo naye Leonsi Kimario akaja na hoja ya kuisihi serikali, kuandaa
utaratibu mzuri wa matumizi na mapato ambayo yamekuwa yakitokana na kodi za
wananchi tofauti na sasa, ambapo kumekuwa kukitokea kashfa za matumizi mabaya ya
fedha yakiwa yanazungumzwa mara kwa mara Bungeni.
Kimario aliendelea kufafanua kuwa endapo utaratibu huo
utaachiliwa uendelee kulitafuna taifa hili, ipo hatari ya walipa kodi kuanza
kugomea ulipaji wake hali ambayo itasababisha serikali kukosa mapato na
kusababisha jamii yenye kipato duni, kuteseka kutokana na hata kukosa huduma za
matibabu na mahitaji mengine muhimu ya kibinadamu ambayo serikali inapaswa
kutoa huduma.
Awali akitoa maelekezo ya taratibu za ulipaji wa kodi
hiyo kwa kutumia mashine za kielektroniki Afisa elimu kwa umma (TRA)
mkoani Ruvuma, Justine Kititi pamoja na mambo mengine aliwataka walipa kodi wilayani
humo, kuzingatia maelekezo ya ulipaji wa kodi ikiwa ni juhudi a kuinua pato la
taifa.
Alifafanua kuwa faida za wafanyabiashara
hao kutumia mashine hizo ni pamoja na kuwasaidia kutunza kumbukumbu katika
biashara zao.
Akizungumzia upande wa hasara ambazo wanaweza
kuzipata endapo watashindwa kuzitumia alieleza kuwa watapata hasara kwa
kulipa kodi kubwa, pale watakapofanyiwa makadirio.
Hata hivyo
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wilaya ya Tunduru Joshua
Mwakatumbula alisema kwa sasa serikali haifanyi biashara, isipokuwa imetafuta
wadau wa kushirikiana nao na mamlaka hiyo, kwa kutengeneza na kuuza mashine
hizo kisha kuzisambaza kwa walengwa yaani wafanyabiashara.
No comments:
Post a Comment