Waziri Mkuu Mizengo Pinda. |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
TAARIFA ya Mkaguzi wa ndani juu ya hoja zilizojitokeza katika
kikao cha fedha, mipango na uongozi kilichoketi Septemba 25 mwaka huu wilayani
Mbinga mkoa wa Ruvuma, na kuwasilishwa katika kikao cha baraza la madiwani la wilaya
hiyo Oktoba 27 mwaka huu, imeendelea kukosolewa na wadau mbalimbali wa elimu
wilayani humo wakisema kwamba ni mpango mbovu ambao ulisukwa na watu wachache wenye
ni mbaya ya kurudisha nyuma maendeleo katika sekta ya elimu, licha ya kila
kilichoelezwa kwenye taarifa hiyo kilikwishapitishwa kwenye vikao halali vya
halmashauri ya wilaya hiyo.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo Hussein
Ngaga ndiye anayenyoshewa kidole akidaiwa kuwa na kundi la watu wachache, ambao
wanaelezwa ndiyo vinara wa kusuka mpango huo ambao sasa umefikia katika hatua
ambayo inaleta mgogoro ambao hauna tija kwa wanambinga.
Ngaga katika taarifa hiyo ametoa hoja saba za kumtuhumu Afisa
elimu wake wa idara ya elimu msingi Mathias Mkali kwamba, amefanya ukiukwaji
mkubwa wa sheria, kanuni na taratibu za fedha za utumishi wa umma, jambo ambalo
tumelifanyia utafiti na kubaini sio kweli badala yake ni mambo ambayo
yalikwisha kubaliwa na kupitishwa kwenye vikao halali. (nakala tunazo)
Katika hali ya
kushangaza, taarifa hiyo iligawiwa kwa madiwani katika baraza hilo ambayo imesainiwa
na mkurugenzi huyo, ghafla Wajumbe husika (Madiwani) baada ya taarifa hiyo kumaliza
kusoma mkaguzi wa ndani, Laston Kilembe walinyang’anywa huku mkurugenzi akisimama
mbele ya kikao na kueleza kuwa haijakamilika watapatiwa tena katika kikao
kijacho cha baraza hilo.
Hali hiyo iliyojitokeza wengi wao walikuwa wakihoji inakuwaje
baraza linaletewa taarifa ambayo haijakamilika, huku wengine wakisema huenda
ndio ulikuwa mpango wenye kubeba matakwa binafsi ambayo hayana tija kwa jamii.
Walisema kuwa wanachotambua siku zote, jambo ambalo
limefanyiwa upembuzi yakinifu na kufikia maamuzi ya kutolewa katika baraza la
madiwani maana yake ni kwamba, lilikwisha kamilika katika kufanyiwa kazi na sio
kulileta nusunusu kitendo ambacho kinatia shaka kati ya utendaji kazi wa mkurugenzi
mtendaji na mkaguzi wake wa ndani kwa kile kinachoelezwa kuwa, huenda ni mpango
wao binafsi wenye kutaka kuharibu mwenendo na makubaliano husika ambayo yalikwisha
pitishwa kwenye vikao halali.
Walifafanua kuwa ni vyema mkaguzi wa ndani Bw. Kilembe
akafanya kazi kwa misingi yenye kujali maslahi ya taifa, kama miongozo yake ya
kazi inavyomtuma na sio kutoa taarifa ambazo hazijakamilika na zenye kuleta
sintofahamu ambayo baadaye huleta shida na kujenga makundi yasiyokuwa ya
lazima.
Utafiti uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa,
hoja za mkaguzi huyo wa ndani hazina mashiko, huku ikibainika kuwa tuhuma
nyingi alizozitoa mbele ya baraza hilo ni makubaliano ambayo yalikwisha pitishwa
na kuridhiwa katika vikao halali vya
baraza la madiwani.
Kilembe katika kikao hicho cha baraza la madiwani, alizua
gumzo ndani ya baraza hasa pale baadhi ya madiwani walipohoji kuwa taarifa yake
kwa nini haina majibu ya upande wa pili wa mtuhumiwa, yaani Afisa huyo wa elimu
msingi wa wilaya ya Mbinga Bw. Mkali.
Walisema, kutoa kwa taarifa yake ya upande mmoja ambayo haina
majibu ya upande wa pili wa mtuhumiwa, ni kutotenda haki na ndio maana madiwani
walishindwa kuunga mkono na kubakia kuleta gumzo ndani ya baraza.
Katika kikao hicho cha baraza la madiwani hata Katibu tawala
wa wilaya ya Mbinga Stephano Ndaki na mkurugenzi wake Hussein Ngaga, kwa
nyakati tofauti walinukuliwa wakisema kwamba suala hilo litaundiwa tume ya
uchunguzi jambo ambalo utekelezaji wake haujafanyika hadi sasa, huku baadhi ya
wadau wakiendelea kuhoji na kusema kauli zao ndani ya baraza hilo zilikuwa ni danganya
toto na maneno ya kupumbaza watu.
Hata hivyo endelea kufuatilia mtandao huu tutachapisha
taarifa yote ya mkaguzi huyo wa ndani, ambayo ilisomwa katika baraza na imesainiwa
na mkurugenzi huyo na baadaye Madiwani walinyang’anywa kwa madai kwamba
haikukamilika, huku wengi wakihoji kama haikukamilika kwa nini ililetwa kwenye
baraza hilo na kuwasilishwa.
No comments:
Post a Comment