Hawa Ghasia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) |
Mbinga.
MAPYA yanaendelea kuibuka katika Halmashauri ya wilaya ya
Mbinga mkoani Ruvuma, ambapo baadhi ya Wafanyakazi wenye mikataba ya ajira ya muda
wamemlalamikia Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Hussein Ngaga,
kwamba amekuwa ni mtu wa kuwatolea lugha zenye kukatisha tamaa ya kufanya kazi na
kutowalipa mishahara yao kwa wakati.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti huku wakiomba majina yao
yasitajwe kwa kuhofia usalama wa kazi zao wakidai kufukuzwa kazi, walisema
Mkurugenzi huyo amekuwa akiwatolea lugha zenye ukali hasa pale wanapokuwa
wakidai madai yao ya msingi, kama vile fedha za malipo ya kazi walizofanya.
Wengine walifafanua kuwa hata mishahara yao ambayo inabidi
walipwe tarehe husika za mwisho wa mwezi, kwa mujibu wa taratibu na sheria
zilizowekwa na serikali, Ngaga amekuwa hafanyi hivyo badala yake amekuwa akiwalipa
kwa kuchelewesha.
“Mkurugenzi huyu anakera sana, hata sisi wafanyakazi wa chini
ambao tumeajiriwa kwa mikataba ya muda katika halmashauri hii, wakati mwingine
mishahara yetu amekuwa akipitiliza tarehe za kutulipa, malipo amekuwa
akiyatekeleza wakati mwingine kwa mwezi unaofuata tarehe 14 hadi 15”, walisema.
Kadhalika waliongeza kuwa katika kipindi cha nyuma kabla ya
Mkurugenzi huyo kuhamia katika halmashauri hiyo ya Mbinga, walikuwa wakilipwa madai
yao kwa wakati na kuwafanya wafanye kazi kwa moyo, licha ya kulipwa mishahara
midogo kulingana na elimu waliyonayo.
Walidai kwamba hata mikataba ya nyuma kabla ya yeye kuwasili
hapa Mbinga, ilikuwa inawaruhusu kukopa fedha katika taasisi za fedha kama vile
benki, lakini alipoingia yeye amebadilisha utaratibu na sasa maisha yao
yamekuwa magumu kutokana na kushindwa kumudu gharama za maisha.
Wafanyakazi wanaomlalamikia mkurugenzi Ngaga ni wa kada ya
Madereva, Walinzi, na Wahudumu wa usafi (Mazingira) ambao baadhi yao wamekuwa
wakifanya kazi kwa kuingia mikataba ya miezi mitatu mitatu na kwamba kila baada
ya miezi hiyo, mwajiriwa hujaza makubaliano mengine.
Utafiti uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umegundua hata
katika mikataba hiyo ambayo nakala yake tunayo, inakataza kuwa Mwajiriwa huyo haruhusiwi
kukopa fedha au kitu chochote katika taasisi yoyote ya fedha, kwa udhamini wa
halmashauri ya wilaya ya Mbinga.
Vilevile mwajiriwa katika kipindi cha kutekeleza mkataba
wake, atakatwa fedha za mafao na Mfuko wa Pensheni ya Watumishi wa Serikali za
Mitaa (LAPF) ambazo atalipwa baada ya kwisha au kusitisha makubaliano husika
yaliyomo ndani ya mkataba, ambapo mwajiriwa atatakiwa pia kutoa taarifa ya
kwisha kwa makubaliano yake katika mfuko huo na kuomba mafao yake.
Mkurugenzi mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Bw.
Ngaga alipotafutwa ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya malalamiko hayo wakati
habari hizi zinaingia mitamboni, simu yake haikupatikana na taarifa
zilizotufikia kutoka kwenye vyanzo vyetu vya habari vilituthibitishia kwamba
yupo safarini nje ya wilaya hiyo.
No comments:
Post a Comment