Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. |
SIKU zote misingi ya taifa linalojali maisha ya wananchi wake
ni ujenzi bora wa elimu, afya na miundombinu inayokuza uchumi huku viongozi
wake katika eneo husika hutakiwa kuwa makini, kujenga mshikamano na kuacha
migogoro ya hapa na pale.
Wahenga wetu husema, ukiona kiongozi muda mwingi amekuwa
akiendekeza migogoro basi tambua kwamba, mahali pale ameshindwa kutawala na
maendeleo hayawezi kupatikana badala yake serikali, inashauriwa kuchukua hatua
za haraka katika kunusuru hali hiyo ili wananchi wake wasipate mateso.
Kinyume chake kukosekana kwa kiongozi wa kweli na asiyejali
utawala bora au maslahi ya wananchi, kunanyima watu fursa ya kufanya maamuzi sahihi
kuhusu rasilimali zao, ikiwemo hata kujiondoa katika lindi la umasikini
unaonuka.
Popote pale kiongozi wa namna hii, ni sawa na kusema ni kiongozi
muflisi ambaye hutambulika muda mwingi kupenda kuruhusu mianya ya rushwa
kutawala kila kona, hasa wakati wa utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi anaowaongoza.
Katika makala haya napenda kuelezea juu ya kilio cha baadhi
ya wananchi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, dhidi ya Mkuu wao wa wilaya Senyi
Ngaga na Mkurugenzi wake Hussein Ngaga, jinsi gani wanavyoiyumbisha wilaya hiyo
na kufikia hatua wananchi kukosa imani nao.
Nimefikia hatua ya kuliweka jambo hili hadharani kutokana na
mambo kadhaa yanayokera wananchi ambayo viongozi hawa, wamefikia sasa kuchukiwa
na watu wanaowaongoza kutokana na kile kinachoelezwa kuwa kupenda kufanya mambo
ambayo hayana msingi katika mustakabali mzima, wa maendeleo ya wananchi wa
wilaya hiyo.
Jambo la kwanza, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali ambavyo
vimetoa ushirikiano wa karibu kwa mwandishi wa makala haya, vimeeleza kuwa mkuu
wa wilaya hiyo ameshindwa kukemea mgogoro ambao unaendelea kufukuta kwa muda
mrefu kati ya mkurugenzi huyo na afisa elimu msingi wa wilaya hiyo, Mathias
Mkali.
Aidha wanaongeza kuwa licha ya afisa elimu huyo kuonekana
kufanya kazi zake vizuri katika kuboresha kiwango cha taaluma wilayani humo,
cha kushangaza viongozi hao wamekuwa wakimpiga vita pasipo sababu yoyote ya
msingi na kusababisha kuwepo kwa tabaka kubwa, ambalo linaitafuna wilaya kwa
kurudisha nyuma maendeleo katika sekta hiyo muhimu.
Wanasema mkuu wa wilaya Ngaga, kukaa kwake kimya pamoja na serikali
kukemea migogoro kazini huenda akawa amejenga maslahi yake binafsi, na kusahau
jukumu alilopewa na Rais Jakaya Kikwete, wakati anamteua kwenda kutumikia
wananchi wa wilaya hiyo kwa kuzingatia kuepuka misingi ya itikadi, rangi au
dini na mambo mengine ambayo hayana tija katika jamii.
Wengi kwa nyakati tofauti wanasema, vitendo vinavyofanywa na
mkurugenzi huyu huku mkuu huyo wa wilaya kutoingilia kati na kukemea, ni sawa
na kushughulika kukomoa wananchi badala ya kubuni na kusimamia maendeleo kwa
faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Senyi Ngaga namfahamu vizuri, ni dada yetu ambaye wananchi wa
Mbinga tulikuwa na imani naye katika kujenga mshikamano wa kuweza kusukuma
mbele gurudumu la maendeleo, lakini kwa haya yanayoendelea sasa anakatisha tamaa
wananchi anaowaongoza.
Wananchi wamefikia hatua ya kuiomba serikali kuingilia kati
juu ya tatizo hili ambalo linaonekana kuwa sugu, ili kuweza kupata suluhu
katika sekta hiyo muhimu ya elimu ambayo sasa kuna dalili tosha za kushuka kwa
elimu wilayani humo, kutokana na mgogoro huo kufikia hatua mbaya.
Nakumbuka mnamo mwezi Juni
1990 aliyekuwa Katibu mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ambao baadae
umekuwa umoja wa Afrika (AU) Edem Kadjo alisema,
“Waafrika kimsingi wanachohitaji ni mambo makuu matatu………uwajibikaji, uwazi na
ushiriki kamilifu katika mambo ya kimaendeleo.
Hivyo basi, viongozi kutozingatia mambo haya matatu huenda kukasababisha
hali ngumu ya maisha kwa wananchi wa eneo husika au taifa kwa ujumla, na kujiandikia
historia mbaya itakayowafanya sisi watawala hususani katika wilaya hii, kwa
wakati huo kutotamani kuandikwa hata kwenye kumbukumbu.
Siku zote nimekuwa nikijiuliza kwamba, kibuli hiki kwa
mkurugenzi huyu wa Mbinga kila kukicha kulumbana na viongozi wenzake wa ngazi
ya chini anakipata wapi?, hata madiwani wake ambao ndio wawakilishi wa wananchi
na wenye kuunda baraza la madiwani, muda mrefu wamekuwa wakilalamikia kuwa
hataki kuwaheshimu hasa pale wanapojenga misimamo yenye maslahi ya wananchi wa
Mbinga.
Hivi karibuni baadhi yao ambao ni wajumbe wa kamati ya
mipango na fedha wamefikia hatua ya kugoma na kutoka nje ya vikao, kutokana na
mkurugenzi huyo kujenga ubishi na kulazimisha mambo ambayo hayana ukweli, kwa kile
kinachoelezwa kuwa anafanya hivyo kwa faida ya matakwa yake binafsi.
Wanasema wanachukizwa na malumbano yanayoendelea sasa kati ya
vigogo hao na watendaji wa chini, ambapo muda mwingi mkurugenzi Ngaga amekuwa
akifikiria kupanga safu katika idara husika na kuhamisha wakuu wa idara
waliokuwepo awali.
“Mkuu wa wilaya tunatambua ndiye mhimili mkuu wa wilaya
katika kumwakilisha Rais, inatushangaza kuona mambo haya yanavyokwenda mrama kila
kukicha huku akiyakalia kimya, hivi tunahoji hakuna mambo ya kimaendeleo ambayo
yeye na mkurugenzi wake wanapaswa kuyafanya kwa manufaa ya wanambinga?, wanahoji.
Ninachoweza kusema katika hili ni vizuri sasa ufike wakati
hakuna sababu ya kuendelea kufumbiana macho tukaze kamba na kujenga misimamo
imara, kwa kuendelea kupiga vita tabia hii ambayo dhahiri inaonesha wazi kutupeleka
kubaya na ni vyema wahusika, wakachukuliwa hatua za kinidhamu kwa lengo la kukomesha
hali hiyo.
Jambo la pili ni kwamba, madiwani wa halmashauri ya wilaya ya
Mbinga wanalalamikia juu ya suala la ujenzi wa maabara kwa shule za sekondari za
serikali wilayani humo, ambapo wanasema badala ya kufanya ujenzi wa majengo
mapya kama alivyoagiza Rais Kikwete, mkuu wa wilaya hiyo kwa kushirikiana na
mkurugenzi wake wameamua kugeuza baadhi ya majengo yaliyokuwa yakitumika
kusomea watoto na kuyafanyia ukarabati kuwa vyumba vya maabara.
Wanasema wao wanatambua kuwa agizo la serikali lilikuwa ni kujenga
majengo mapya ya maabara na sio kufanya hiki kilichofanywa hapa Mbinga, ambapo
wameeleza kuwa kutokana na shule nyingi za sekondari wilayani humo kuwa na
upungufu wa madarasa ya kusomea watoto, jambo hilo lililofanywa litaleta shida
na kufanya watoto wakose mahali pa kusomea.
Utafiti uliofanywa na mtandao huu umebaini kuwa halmashauri
ya wilaya ya Mbinga ina jumla ya shule za serikali 38, ambapo robo tatu ya shule
hizi badala ya kufanya kazi ya ujenzi wa majengo mapya ya maabara uongozi wa
wilaya hiyo umefanya maamuzi ya kuchukua vyumba vya madarasa vilivyopo tokea
awali, na kuvikarabati wakivifanya ndio vyumba vya maabara kwa masomo ya
sayansi huku idadi ya wanafunzi husika waliokuwa wakitumia kusomea katika
vyumba hivyo wakikosa sehemu ya kuendelea na masomo.
Kufuatia hali hiyo wanafunzi wamekuwa wakilazimika
kulundikana katika majengo machache yaliyopo, huku wazazi wakisema wanahofia
uwingi wa watoto waliomaliza elimu ya msingi mwaka huu, ambao wamefaulu kwenda
kuanza kidato cha kwanza mwakani katika shule hizo wakisema hilo ni tatizo ambalo
litaleta adha kubwa, hivyo ni vyema njia mbadala ikatafutwa haraka ili kunusuru
hali hiyo.
Nimezungumza na baadhi ya wananchi na wanafunzi mashuleni kwa
nyakati tofauti ambao waliomba majina yao yasitajwe, wanasema wao wanachotambua
baada ya serikali kutoa agizo hilo la ujenzi wa vyumba vya maabara, mkuu wa
wilaya na mkurugenzi wake wangefanya utaratibu wa kuhamasisha wananchi
kuchangia nguvu zao kama ilivyofanyika kwa ujenzi wa shule hizo, na sio kufikia
hatua ya kukarabati majengo yaliyopo.
Wanasema katika kuandaa taarifa zao wasije wakathubutu
kumdanganya Rais Kikwete kwamba wamejenga majengo mapya ya maabara, wakati
shule nyingi wametumia mtindo wa kukarabati madarasa waliyokuwa wakisomea
wanafunzi, na kugeuza kuwa chumba cha maabara jambo ambalo linapingana na agizo
la serikali la ujenzi wa majengo mapya.
Jitihada ya kumpata mkuu wa wilaya ya Mbinga aweze
kuzungumzia juu ya malalamiko haya, hakuweza kupatikana ofisini kwake huku simu
yake ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa, na kwamba hata mkurugenzi wake
alipokuwa ametembelewa na waandishi wa habari alikuwa akisema “nenda kaandikeni tu”, huku akikataa kutoa ufafanuzi wowote
juu ya malalamiko hayo ambayo yapo bado mbele yake.
Binafsi nasema, fikra za hayati Mwalimu Julius Nyerere na ndoto zake za maendeleo ya
Watanzania aliyotaka kuijenga tumeziweka kapuni, viongozi wetu badala ya
kujenga daraja wanajitahidi kujenga ukuta ambao unatenganisha fikra za mwalimu
na kizazi hiki kipya.
Miaka 25 ya urais wake, sote tunatambua Nyerere aliacha
misingi ya utawala bora kwa kila kitu, hivyo kiongozi kufikia mahali kuendekeza
migogoro kazini na kuacha kutimiza au kugeuza kinyume maagizo ya kimaendeleo
unayopewa na kiongozi wako wa ngazi ya juu, ni sawa na kuleta hasara isiyokuwa
na maslahi kwa umma na ukibainika kufanya hivi ni vyema vyombo husika vichukue
mkondo wake wa kukuwajibisha ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
No comments:
Post a Comment