Waziri Mkuu Mizengo Pinda. |
Na
Mwandishi wetu,
Mbinga.
TUME
ya watu wawili ambayo imeundwa na serikali, kwa ajili ya kuja kuchunguza
mgogoro uliopo kati ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga
mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga na Afisa elimu msingi wa wilaya hiyo, Mathias
Mkali imetiliwa shaka huku ikinyoshewa kidole na kudaiwa kutotenda haki kutokana
na tume hiyo kuonekana ikiegemea upande wa mkurugenzi huyo.
Baadhi
ya wadau wa elimu wakiwemo na watendaji wa serikali, ambao wameteuliwa kwa ajili ya kuhojiwa walisema hayo mjini
hapa, wakati walipokuwa wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wetu
mara baada ya kufanyiwa mahojiano na tume hiyo.
“Mambo
tunayoulizwa ndani ya tume mengi yanaonesha ni yale yale ambayo yametengenezwa
na mkurugenzi, sisi tunapotaka kutoa hoja zetu za msingi tunabanwa sana na
kunyimwa uhuru wa kujieleza kweli hapa kuna haki? au tume hii imekuja kwa ajili
ya kumbeba mtu”, ? walihoji.
Walisema
wanashangazwa kuona wakati mwingine tume imekuwa ikihoji kwa kutumia lugha za
vitisho, zenye kuonyesha kubeba kundi la upande mmoja na kwamba chumba cha
mahojiano kilichopo katika jengo la ukumbi mdogo wa halmashauri ya wilaya hiyo,
wahojiwa wamekuwa hawapewi uhuru wa kutosha wakati wa kujieleza jambo ambalo
linajenga kukosa imani nao.
Aidha
walieleza kuwa wanashangazwa kumuona Afisa utumishi wa wilaya ya Mbinga,
Emmanuel Kapinga, kuwepo ndani ya chumba cha mahojiano na tume hiyo ambapo
wakati wa mahojiano muda mwingi amekuwa mtu wa kupinga na kuwa mkali pale
mhojiwa anapokuwa akitoa maelezo yenye ukweli juu ya jambo husika linaloulizwa
kutoka kwa mjumbe wa tume.
Watu
wengi wamekuwa wakihoji, kama tume hiyo imepewa uhuru wa kufanya kazi si jambo
la busara kwa afisa utumishi huyo Bw. Kapinga, kuwepo katika chumba cha mahojiano
na kupinga maelezo yenye ukweli ambayo yanatolewa na wahojiwa hivyo hali hiyo
endapo itaendelea, hapo hakuna uhuru wa tume katika kutenda haki juu ya mgogoro
huu ambao unaendelea kufukuta hadi sasa.
Hali
hiyo walifafanua kuwa ni kunyima uhuru wa wahojiwa namna ya kujieleza kwa yale
mambo muhimu waliyonayo, hivyo kuna kila sababu ya tume hiyo kutiliwa mashaka
kutokana na mwenendo huo unaoendelea
sasa.
Pia
Uchunguzi uliofanywa na mtandao huo umebaini kuwa, tume hiyo hata sehemu ya
malazi wameandaliwa na vigogo wa wilaya hiyo ambapo baadhi ya wananchi wamekuwa
wakihoji kwamba, kitendo hicho kinaashiria kuwepo kwa mianya ya rushwa ambayo itapelekea
haki kutotendeka.
Ikulu
ndogo ya Rais iliyopo wilayani hapa, ndiyo sehemu ambayo tume hiyo imeweka
kambi kwa ajili ya malazi na kwamba nimeshuhudia kumekuwa na mfululizo wa
magari ya baadhi ya vigogo wa ngazi ya juu wa wilaya ya Mbinga hasa majira ya usiku na mapema alfajiri,
wamekuwa wakienda huko kuzungumza nao jambo ambalo ni dalili tosha kwamba kuna
mbinu chafu ambazo zinaendelea kusukwa kwa lengo la kuvuruga ukweli wa jambo
ambalo linachunguzwa.
Mkuu
wa wilaya hiyo Senyi Ngaga, Mkurugenzi mtendaji Hussein Ngaga, Katibu tawala
Stephano Ndaki na Afisa usalama wa Taifa wa wilaya (Jina tunalo) ndio ambao
wamekuwa mara kwa mara wakionekana kwenda katika Ikulu hiyo, ambako tume hiyo
imeandaliwa malazi.
Wadau
wa elimu wanasema ni vyema tume hiyo ingeachwa huru wakati inapofanya kazi zake
bila kuingiliwa na mtu yeyote, ili mwisho wa siku jamii iweze kupata ukweli juu
ya mgogoro huu uliopo kati ya mkurugenzi huyo na afisa elimu wake.
Mwenyekiti
wa tume hiyo, Philemon Bossy alipozungumza na waandishi wa habari juu ya tuhuma
hizo zinazoelekezwa kwa tume hiyo anayoiongoza, alikana kuwepo kwa mambo hayo
na kusema kuwa wao wamekuja kufanya kazi ya kuchunguza tuhuma zilizopo.
“Sisi
tunapowahoji wahusika ni lazima afisa utumishi naye awepo ndani ya tume, yeye
anakuwa kama shahidi wakati mahojiano yanayoendelea kufanyika kwa sababu
tumekuja kuchunguza mambo ya kiutumishi, hivyo si makosa kwa yeye kuwepo wakati
tunapohoji”, alisema.
Hata
hivyo Philemon aliongeza kuwa hata Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya
ya Mbinga, Hussein Ngaga naye alikuwa akilazimisha awepo ndani ya chumba cha
mahojiano lakini alimkatalia na kumwambia kuwa hatakiwi kuwepo na endapo kama
litafanyika hilo, itakuwa ni tendo la uvunjifu wa taratibu na sheria husika.
No comments:
Post a Comment