Waziri wa TAMISEMI Hawa Ghasia (kulia) pamoja na Katibu mkuu TAMISEMI Jumanne Sagini. (kushoto) |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
KASORO za uchaguzi zilizojitokeza katika
uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika hivi karibuni hapa nchini, pia hali
ya hewa imechafuka wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma kufuatia baadhi ya
Waandikishaji na Wasimamizi wa uchaguzi huo, kumlalamikia Mkurugenzi mtendaji
wa Halmashauri ya wilaya hiyo Hussein Ngaga, kwamba malipo ya posho walizolipwa
katika zoezi hilo amewalipa kidogo, tofauti na maeneo mengine nje ya wilaya
hiyo.
Aidha kufuatia hali hiyo Waandikishaji na Wasimamizi hao wamemuomba Waziri wa
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Hawa Ghasia, kuingilia kati na
kuweza kulifanyia kazi jambo hilo ili waweze kupata haki yao ya msingi kwa kazi
waliyofanya.
Malalamiko hayo yalitolewa kwa nyakati tofauti walipokuwa wakizungumza na
mwandishi wa habari hizi, kwa kuomba majina yao yasitajwe gazetini ambapo
walisema kuwa hata wakati wanafanyiwa semina na kupewa miongozo juu ya
utekelezaji wa zoezi hilo, hawakulipwa posho badala yake waliambiwa kwamba
watalipwa mara baada ya uchaguzi kufanyika.
Kwa mujibu wa mtoa habari wetu alidai kuwa siku ya mwisho ya uchaguzi huo
wamesainishwa fomu ya malipo shilingi 85,000 lakini cha kushangaza fedha
taslimu waliyokabidhiwa mkononi ni shilingi 50,000 tu, jambo ambalo
walipojaribu kuhoji hakuna majibu sahihi waliyopewa.
Waliendelea kudai kuwa maeneo mengine wilayani humo, waandikishaji wamelipwa
shilingi 35,000 kwa siku saba, ambapo kwa siku moja walikuwa wakilipwa shilingi
5,000 jambo ambalo wamekuwa wakilalamika kuwa ni kidogo, tofauti na maeneo
mengine nje ya wilaya hiyo wenzao walikuwa wakilipwa shilingi 10,000 hadi
15,000 kwa siku wakati wanafanya zoezi hilo la uandikishaji wapiga kura.
“Sisi tunasikitishwa na malipo haya kidogo, hata wakati tunafanyiwa semina juu
ya zoezi hili hatukulipwa kitu tulikuwa tunatumia fedha zetu wenyewe za
mifukoni, Mkurugenzi mtendaji alituma taarifa kwetu wakati tunafanyishwa semina
kwamba halmashauri haina fedha zimetumika kwenye mambo ya ukaguzi tumvumilie
atatulipa siku ya mwisho ya uchaguzi na ndivyo alivyofanya”, walisema.
Jitihada ya kumpata Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Bw.
Ngaga ofisini kwake, ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya malalamiko hayo
hazikufanikiwa na simu yake ya kiganjani ilikuwa haipatikani.
No comments:
Post a Comment