Na Gideon Mwakanosya,
Songea.
BAADHI ya wakazi wa
halmashauri ya Manispaa ya songea mkoa wa Ruvuma, wamezilalamikia mamlaka husika zikiwemo kikosi cha usalama
barabarani mkoani humo na Sumatra kwa
kushindwa kudhibiti daladala mbovu, zinazofanya kazi ya kubeba abiria katika
manispaa hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti wakazi hao wameeleza kuwa kwa muda mrefu sasa, daladala ambazo
zinaonyesha kuwa ni mbovu lakini zimekuwa zikiendela kubeba abiria zimekuwa zikihatarisha
maisha ya abiria wanaotumia daladala hizo.
Felix Komba mkazi wa Mahenge
alisema kuwa daladala zinazotoka Songea mjini mtaa wa Delux, kwenda Matogoro na
Songea Boys zinaonekana hata kwa macho kuwa ni mbovu.
Said Athumani mkazi wa eneo
la Matarawe amesema kuwa kwa muda mrefu wakazi wa maeneo hayo, na Mjimwema
wamekuwa wakitumia daladala ambazo ni
mbovu na kwamba zimekuwa zikisheheni abiria, na wakati mwingine zikiwa kwenye
eneo la mlima zinashindwa kupanda.
Ameziomba mamlaka
zinazohusika kusimamia shughuli mbalimbali za vyombo vya moto mkoani humo, kuona
umuhimu wa kuchukua hatua madhubuti na kuzisitisha daladala zote ambazo
zinaonekana hazifahi kubeba abiria.
Kwa upande wake Afisa mfawidhi
wa mamlaka ya udhibiti wa nchi kavu na majini (SUMATRA) mkoani Ruvuma,
Sebastian Rohai alisema kuwa ofisi yake ilishapokea malalamiko kutoka kwa
abiria na tayari zoezi la kukamata daladala mbovu zinazofanya kazi Manispaa ya
songea, zimeshaanza tangu wiki iliyopita.
Kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma
Mihayo Msikhela alisema kuwa tangu abiria walipoanza kulalamikia ubovu wa daladala hizo,
tayari kikosi cha usalama barabarani mkoani humo kimeshaanza kazi ya kukamata
daladala zote ambazo inadaiwa kuwa ni mbovu.
Hata hivyo Mwenyekiti wa
chama cha usafirishaji mkoa wa Ruvuma Golden Sanga, alipohojiwa kuhusiana na
malalamiko ya baadhi ya daladala zinazotoa huduma katika maeneo ya njia za
kutoka soko kuu kwenda Mjimwema, Soko kuu kwenda mkuzo, Delux kwenda Songea
Boys na Delux kwenda Matogoro alisema kuwa ofisi yake kwa kushirikiana na
mamlaka husika inayafanyia kazi malalamiko hayo.
No comments:
Post a Comment