Na Mwandishi wetu,
Dar.
RAIS Jakaya Kikwete hatimaye leo ametengua nafasi
ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna
Tibaijuka kupitia hotuba aliyotoa kuzungumzia kashfa ya upotevu wa fedha
kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.
Hatua hiyo imechukuliwa na Rais
Kikwete mbele ya wazee wa Dar es Salaam, aliokuwa akiongea nao na
matangazo kurushwa moja kwa moja kupitia televisheni ya taifa na vyombo
vingine.
Uchunguzi uliofanywa na kamati ya hesabu za umma ya
Tanzania (PAC) ilidai kuwa Profesa Tibaijuka ni mmoja wa watu
walionufaika kinyume cha sheria, kwa kujipatia fedha zilizotoka katika
akauti hiyo iliyofunguliwa kutunza fedha kusubiri ufumbuzi wa mgogoro wa
kibiashara kati ya kampuni ya kusambaza umeme TANESCO na kampuni
binafsi ya kuzalisha umeme ya IPTL.
Siku chache zilizopita Profesa
Tibaijuka aliitisha mkutano na waandishi wa habari Jijini Dar Es Salaam,
kubainisha kuwa hakuwa akikusudia kujiuzulu kutokana na tuhuma
zilizokuwa zikimkabili.
Aidha Rais Kikwete hakutangaza
kuwachukulia hatua watumishi wengine waliodaiwa kuhusika na tuhuma hiyo,
kwa maelezo kuwa uchunguzi zaidi unatakiwa kwa kila mtuhumiwa.
Kumekuwa
na ubishi mkubwa kujadili endapo fedha ambazo ni mabilioni
zilizochukuliwa zilikuwa za umma au la.
Hata hivyo Rais Kikwete alisema
maelezo aliyopewa na wataalamu yanaonyesha hazikuwa mali ya TANESCO.
No comments:
Post a Comment