Hussein Ngaga, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
AGIZO lililotolewa hivi karibuni na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya
wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga juu ya michango wanayochanga wazazi
kwa ajili ya watoto wao kujisomea wakati wa likizo (Makambi) wilayani humo, na kuingizwa
kwenye akaunti ya fedha za ruzuku kutoka serikalini kwa ajili ya kuendeshea
mitihani mashuleni (Capitation) limezua mapya, kufuatia kamati husika
zinazojishughulisha na uendeshaji wa makambi hayo kulalamika wakidai kwamba, kufanya
hivyo ni ukiukaji wa taratibu na makubaliano yaliyofanywa na wazazi kupitia
vikao husika.
Imeelezwa kuwa ni vyema mkurugenzi huyo, akazingatia mawazo na makubaliano yaliyofanywa na
wazazi hao na sio vinginevyo, hivyo kutozingatia hilo ni kukosa utawala bora katika
jamii na kuleta migogoro isiyokuwa ya lazima.
Kwa nyakati tofauti walipozungumza na mwandishi wa habari hizi wajumbe wa
kamati hizo walieleza kuwa, michango inayokusanywa kutoka kwa kila mzazi ambaye
ana mtoto anayesoma katika shule husika, hukabidhiwa mkuu wa kambi na kamati hufanya kazi ya
kupanga mapato na matumizi na sio utaratibu huo ambao mkurugenzi huyo ameutoa.
Walidai kuwa michango hiyo kuingizwa kwenye akaunti ya Capitation hivi
sasa kunaleta kikwazo kikubwa kwao, hasa pale wanapohitaji kufanya matumizi
husika kwani wanapokwenda kwa mkurugenzi huyo ili waweze kupata fedha hizo kwa
ajili ya kuendeshea shughuli za watoto hao katika kambi, hukumbana na vikwazo
vingi.
Walifafanua kuwa uendeshaji wa makambi hayo ni mfumo ambao wazazi wa
wilaya hiyo walijiwekea mikakati yao wenyewe na kujenga makubaliano juu ya
namna ya kuinua kiwango cha taaluma, kupitia vikao vya Mabaraza ya kata (WDC)
ambapo makubaliano yao yalikuwa kila mchango unapokusanywa akabidhiwe mkuu wa
kambi husika, kwa ajili ya kupanga matumizi na baadaye mwisho wa kambi taarifa
ya mapato na matumizi itolewe kwenye kikao hicho cha WDC kwa eneo husika.
“Hapa tunavyozungumza kuna baadhi ya wenzetu ambao wameingiza michango hii
kwenye akaunti ya Capitation, wakifuatilia fedha kwa mkurugenzi huyu ili waweze
kwenda vijijini kwa ajili ya kuendeshea makambi, wanashindwa kuzipata kwa muda
muafaka huku wakibaki wanasumbuka hawajui cha kufanya”, walisema.
Vilevile waliongeza kuwa kutokana na ukiritimba huo wa ucheleweshaji wa
kutoa fedha kwa wakati kunasababisha baadhi ya makambi mashuleni, huko vijijini
watoto hulala na giza katika eneo ambalo wameweka kambi, kutokana na kukosa fedha za kununua mafuta (Petroli) kwa
ajili ya kuweka kwenye genereta.
Kutotolewa fedha hizo kwa wakati na kukosekana kwa mafuta hayo, watoto
hao hivi sasa huko vijijini wanashindwa hata kujisomea nyakati
za usiku, jambo ambalo walimu wengi wamesema kuwa huenda utaratibu huo aliouanzisha
mkurugenzi Ngaga juu ya fedha hizo kuingizwa kwenye akaunti hiyo ya fedha za
ruzuku kutoka serikalini, badala ya kukabidhiwa mkuu wa kambi husika na kupanga
taratibu za matumizi ya kuendeshea masomo ya watoto wakati wa likizo kama
ilivyokuwa awali, ndio mwelekeo wa kufa kwa makambi hayo na wilaya ya Mbinga huenda
ikawa nyuma kielimu kwa shule za msingi kutokana na walimu wengi kuanza kukata tamaa
ya kujitolea kufundisha.
Pia nimezungumza na Wazazi kwa nyakati tofauti nao walisema, wanamshangaa
Mkurugenzi huyo kuanzisha taratibu za kwake bila kushirikisha wazazi wenye
watoto kupitia vikao husika, ambapo walifafanua kuwa makubaliano yao kupitia
vikao vya WDC haikuwa hivyo huku baadhi yao wakisema ni vyema mfumo wa
kujisomea watoto wakati wa likizo, taratibu husika akaziacha kama wazazi
walivyokubaliana katika vikao hivyo na sio kuzibadilisha ambapo asipofanya
hivyo mbele wanaona giza kwa maendeleo ya watoto wao kielimu wilayani humo.
“Kiongozi mzuri ni yule ambaye anashirikisha wenzake na sio kuamua mambo
yeye binafsi, kwa jambo hili tunamtaka afuate taratibu ambazo sisi wazazi kwa
kushirikiana na walimu wetu kupitia vikao husika, tulikwisha kaa na kuweka
mikakati madhubuti ya kufanikisha watoto wetu wakue kielimu hivyo tunasema
hatuhitaji kurudishwa nyuma na mtu yeyote ambaye hana uchungu na maendeleo ya
wanambinga”, walisema.
Walieleza kuwa michango wanayochanga wazazi kwa watoto wao ili
wajisomee wakati huo wa likizo, sio mpango uliowekwa na serikali bali ni
makubaliano yao na walimu mashuleni ambapo kufikia hatua ya kuingiza fedha hizo
kwenye akaunti ya serikali ni kuingilia matakwa yao ambayo wamejiwekea wenyewe, hivyo
wamemtaka aache kufanya hivyo badala yake afuate makubaliano ya vikao husika vya
mabaraza ya kata.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Hussein Ngaga
alipotafutwa ili aweze kuzungumzia malalamiko hayo, hakuweza kupatikana na simu
yake ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa.
No comments:
Post a Comment