Saturday, December 20, 2014

MKURUGENZI MTENDAJI MBINGA AMDANGANYA RAIS KIKWETE, ADAIWA KUCHOTA FEDHA ZA WAKULIMA WA KAHAWA NA KUZIPANGIA MATUMIZI KINYUME NA TARATIBU ZA USHIRIKA

Rais Jakaya Kikwete.

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

SHILINGI bilioni 2 ambazo baadhi ya vyama vya ushirika wa kahawa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, vilikopeshwa hivi karibuni na shirika la hifadhi ya jamii (NSSF) zimezua malalamiko kwamba, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Hussein Ngaga hakuzipeleka kwenye vyama hivyo badala yake anadaiwa kuziingiza kwenye akaunti ya halmashauri ya wilaya hiyo na kuanza kukopesha vikundi husika.

Imeelezwa kuwa kitendo kilichofanywa na mkurugenzi huyo, ni ukiukwaji wa sheria na taratibu za ushirika, hivyo alitakiwa fedha hizo azifikishe kwanza kwenye ushirika kwa kufuata mgawo husika na sio yeye kuzipangia matumizi na kwamba kwa kufanya hivyo, amemdanganya Rais Jakaya Kikwete kwa kauli yake aliyoitoa hivi karibuni mbele yake kwamba fedha hizo watakabidhiwa walengwa wa vyama vya ushirika.

Rais Kikwete mnamo Julai 19 mwaka huu, alikabidhi mfano wa hundi kwa viongozi wa vyama vya ushirika ambavyo vilikopeshwa fedha hizo alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo, kwa vyama vinne ambavyo vilipewa mkopo huo na shirika hilo.


Vyama vinne vya ushirika ambavyo vilipatiwa mkopo huo ni Mahilo, Ngaka, Ngima na Pilikano ambapo hujishughulisha na uzalishaji wa zao la kahawa wilayani humo, na kila kimoja ilibidi kipewe shilingi milioni 500 lakini mkurugenzi Ngaga hakupeleka fedha hizo kwenye vyama hivyo badala yake alitengeneza utaratibu anaoujua yeye na kuvipatia fedha kidogo kidogo kulingana na kiasi cha kahawa, inayoingizwa kiwandani kwa ajili ya kukobolewa.

Baadhi ya watumishi wa halmashauri ya wilaya hiyo (majina tunayo) walionekana muda mwingi wakitumia magari ya halmashauri kutia mafuta ambayo ilibidi yakafanye shughuli nyingine za maendeleo ya wananchi vijijini, wakilipana posho na kufanya ufuatiliaji kuhakikisha kwamba vikundi vinapeleka kahawa kiwandani ndipo vinakopeshwa fedha, jambo ambalo watu wengi walikuwa wakihoji inakuwaje halmashauri inaingia katika biashara ya kahawa?

Wakulima wa vyama hivyo vya ushirika walipozungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, walidai kuwa huenda Mkurugenzi huyo alifanya hivyo akiwa na makusudi yake binafsi, ili fedha hizo aweze kunufaika nazo kwa namna moja au nyingine na sio mkulima kama shirika la NSSF lilivyo lenga.

Walidai kuwa pamoja na fedha hizo kulenga kumpunguzia mkulima wa kahawa makali ya maisha, bado hawaoni tofauti kama ilivyo kwa makampuni binafsi ambayo yalikuwa yakinunua kahawa tena kwa bei inayoridhisha.

Baadhi ya wakulima ambao walikopeshwa fedha hizo walisikitishwa na kitendo hicho, wakieleza kuwa wao wanachoelewa ni kwamba fedha hizo ilibidi ziingizwe kwenye akaunti za vyama vyao vya ushirika na wanachama kupitia uongozi wao, kujipangia taratibu za kukopeshana kulingana na kiasi cha kahawa walichonacho.

Aidha waliongeza kuwa licha ya fedha hizo, na NSSF kukopesha kwa riba nafuu ya asilimia 9 bado mkulima huyo kwa malipo ya kwanza alilipwa shilingi 2,500 na ya mwisho shilingi 2,000 jambo ambalo wanamashaka nalo, kwani makampuni binafsi yamekuwa yakinunua kahawa kwa mkulima shilingi 4,800 hadi 5,000 na yamekuwa yakilipa riba kubwa benki ya asilimia 24.

Wengi wao wamekuwa wakihoji inakuwaje mkopo huo wa riba nafuu, uliotolewa na shirika hilo, mkulima alipwe fedha kidogo tofauti na bei inayolipwa na makampuni binafsi kwa wakulima, ambapo hukopa fedha benki kwa riba kubwa?

Lengo la fedha hizo kutolewa na shirika hilo la hifadhi ya jamii, lilikuwa ni kutoa mikopo yenye gharama nafuu kwa wakulima wadogo wadogo wilayani Mbinga, ambao wamejiunga kisheria katika vikundi hatimaye waweze kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini.

Pia wakulima hao waondokane na changamnoto ya kukosa uhakika wa huduma za afya, ununuaji wa pembejeo ili waongeze uzalishaji na uhakika wa kipato baada ya kufikia umri wa uzee, ambapo husababisha kushindwa kuendelea na shughuli za kilimo.

Hata hivyo jitihada ya kumpata Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Bw. Ngaga ofisini kwake ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya malalamiko haya hazikufanikiwa na simu yake ya kiganjani ilikuwa haipatikani.


No comments: