Msanii Gidion Kabrother akisisitiza jambo, wakati alipokuwa akizungumza na Mkurugenzi wa mtandao huu, Kassian Nyandindi Mbinga mjini mkoa wa Ruvuma. |
Hii ni moja kati ya Filamu yake ambayo aliitoa mara ya mwisho, ikitamba kwa jina la Ni Shida, ambayo ipo sokoni. |
Ruvuma.
MUIGIZAJI wa filamu nchini, Gidion Simon maarufu kwa
jina la Kabrother anatarajia kutoa filamu yake mpya yenye picha kali, ambayo
itatamba hivi karibuni kwa jina la Mkuki kwa Nguruwe hivyo wadau mbalimbali amewataka kukaa
mkao wa kula na kuipokea albamu hiyo, kwa kuendelea kumuunga mkono kwa kazi zake.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Kabrother
anasema filamu hiyo inazalishwa na kusambazwa na kampuni ya Pamoja Film,
iliyopo Jijini Dar es Salaam.
Anafafanua kuwa filamu hiyo imebeba maudhui mazuri
yenye kulenga kuelimisha jamii, ikiwemo inakemea vitendo vinavyofanywa na
baadhi ya wafanyakazi mahospitalini wenye tabia ya kutibu wagonjwa, kwa kutumia
madawa ambayo yamepitwa muda wake wa matumizi na kusababisha madhara kwa
mtumiaji.
“Ndugu mwandishi katika matumizi ya madawa haya feki
ni hatari sana, hata mkurugenzi husika mwenye hospitali hujikuta siku ya mwisho
hata ndugu yake akiathirika na madawa hayo kwa sababu tu ya uzembe huu na
kusababisha nguvu kazi ya taifa hili kupotea”, anasema Kabrother.
Pia filamu hiyo inaiasa jamii hasa kwa wale wenye
kipato, kuacha tabia au matendo ya kuumiza wenzao kwa namna moja au nyingine
kutokana tu, na hali ya uchumi mzuri walionao.
Kabrother uzoefu wake katika fani ya uigizaji wa
filamu hapa nchini, amepitia kwenye vikundi vya sanaa vya Tamacaefo sunlight
(Manyoni), Emima (Morogoro) na Best tallent (Shinyanga).
Kwa sasa anafanya kazi zake za usanii kwa kushirikiana
na wasanii wakongwe hapa nchini Senga, Pembe, Kinyambe na Matumaini na kwamba
Kabrother anatamba na filamu zake tatu ambazo tayari zipo sokoni zenye
kufahamika kwa majina ya Exccident, Nimeshindwa na ile iitwayo Ni shida.
Pamoja na mambo mengine Gidion Kabrother licha ya kuwa
msanii, pia ni mwalimu wa shule za msingi ambaye amebobea kwenye masomo ya
Hisabati, Kingereza na Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT).
Kadhalika ni mtaalamu wa michezo ya mpira wa mikono
(Hand ball) na mpira wa wavu (Volley ball), na kwamba kwa mtu yeyote yule ambaye
anahitaji kupata filamu zake anaweza kufanya mawasiliano kwa kupiga simu ya
kiganjani namba; 0757 947301.
No comments:
Post a Comment