Gaudence Kayombo. |
Mbinga.
BAADHI ya Wakazi wa mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wamemtaka
Mbunge wa jimbo la Mbinga, Gaudence Kayombo kufuta kauli zake anapokuwa akihutubia
wananchi katika majukwaa ya kisiasa na kujenga hoja za kuwatetea Mkurugenzi
mtendaji Hussein Ngaga na Mkuu wa wilaya hiyo, Senyi Ngaga kwamba ni viongozi
wazuri na wameleta maendeleo makubwa wilayani humo.
Sambamba na hilo wananchi hao ambao ni wapiga kura wake,
wamesema kuwa kauli za Kayombo kuwatetea viongozi hao ni sawa na kujichimbia
kaburi kwa kupoteza nafasi aliyonayo, katika uchaguzi mkuu ujao ambao unatarajiwa
kufanyika mwakani kwa nafasi ya kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani.
Walifafanua kuwa wanamshangaa Mbunge huyo amekuwa
akiwasafisha viongozi hao wawili kwamba wanafanya vizuri, wakati maendeleo
mengi yaliyofanywa wilayani humo yamefanywa na viongozi wenzao waliowatangulia
na sio wao ambao wamefika hapa wilayani wanamuda mfupi na hakuna jambo jipya la
maendeleo walilobuni na kuweza
kujivunia kwa wananchi wakati mengi yaliyopo wanayoyaendeleza
ni yale ambayo yalifanyiwa ubunifu na viongozi wenzao waliowatangulia.
Hayo yalisemwa jana na wakazi wa mji wa Mbinga kwa nyakati
tofauti, mara baada ya Mbunge Kayombo kumaliza kuhutubia katika viwanja vya
soko kuu mjini hapa, kwenye mkutano wa hadhara ambao uliandaliwa na Chama Cha
Mapinduzi (CCM) wilayani humo kwa ajili ya kushukuru wapiga kura wake kukipatia
viti vingi vya nafasi ya Wenyeviti wa vitongoji, katika chaguzi za serikali za
mitaa zilizofanyika hivi karibuni.
“Sisi tunamshangaa sana huyu Mbunge, anasimama jukwaani na
kuanza kumsifia mkurugenzi na mkuu wake wa wilaya, ambao dhahiri wameshindwa kuiongoza
wilaya hii, kila kukicha wao wanaendekeza migogoro na wafanyakazi wenzao na
kufikia hatua serikali kutumia fedha nyingi za walipa kodi kuleta tume kuchunguza
mambo ya kijinga ambayo yamesababishwa na hawa watu”, walisema.
Aidha wananchi hao ambao walionekana kukerwa na kauli za Bw.
Kayombo, walisema wana kila sababu za kumnyoshea kidole kwani yeye ndiye anayelea matatizo yanayoendelea
hapa wilayani Mbinga ambayo yanahatarisha ustawi wa maendeleo ya wananchi wake,
kwani hadi sasa ameshindwa hata kukemea na kusimama katikati ili kutenda haki badala
yake anaonekana kuegemea upande wa mkurugenzi na mkuu wa wilaya hiyo.
Wengi walikuwa wanahoji na kusema kwamba, matendo
anayoyafanya Mbunge huyo kwa kukumbatia uozo huu unaoendelea kutafuna kizazi
hiki cha wanambinga ni dhambi ambayo itakuja kumtafuna baadae hapa hapa duniani,
kutokana na watu wengi wamekuwa wakisikitika juu ya mwenendo mbaya anaoufanya
wa kulea na kuficha mapungufu ya vigogo hao hapa wilayani ambayo wamekuwa
wakiyafanya na kuudhi wananchi.
“Huyu Mbunge tunamashaka naye tumekaa naye vikao vingi na
kumweleza matatizo ya hawa anaowatetea leo, lakini hataki kuelewa sasa asubiri mwarobaini
wake uchaguzi mkuu ujao mwakani, kwa sababu tumechoka viongozi anaowasifia kila
kukicha wamekuwa wakizalisha migogoro ambayo haina tija kwetu…………”
Pamoja mambo mengine walieleza kuwa, ni vyema serikali
ikasimama kidete ikatenda haki na kuingilia kati juu ya matatizo na migogoro
iliyopo kazini kati ya vigogo hao wa wilaya, na wafanyakazi wenzao wa ngazi ya chini
katika halmashauri ya Mbinga ili kuweza kunusuru ustawi wa maendeleo ya
wananchi wa wilaya hiyo.
Waliongeza kuwa
hawaoni sababu kwa serikali kuendelea kumfumbia macho Mkurugenzi Bw. Ngaga na Mkuu wa
wilaya Bi. Ngaga, ambao wamekuwa wakitengeneza mifarakano kila kukicha badala
ya kubuni maendeleo.
No comments:
Post a Comment