Na Steven Augustino,
Tunduru.
CHAMA Cha wananchi (CUF) Taifa kimetangaza sera ya
kutoa gawiwo kwa wananchi wake, endapo kitapatiwa ridhaa ya kuongoza nchi
katika uchaguzi mkuu ujao ikiwemo wananchi watanufaika na rasilimali za taifa,
katika kipindi chake cha uongozi.
Aidha kitafungua akaunti maalumu tatu ambapo baadhi ya
mapato yake ndiyo yatakayokuwa yakigawiwa kwa wananchi hao.
Katibu Mkuu wa CUF makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar,
Maalim seif Sharifu alisema hayo alipokuwa akihutubia wananchi wa wilaya ya
Tunduru mkoani Ruvuma, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhamasisha wananchi
kujiunga na chama hicho.
Maalimu Seif, alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni
wakati wake sasa wa kufunga virago na kwenda zake, huku akieleza kuwa CUF kimejipanga
kuchukua vitongoji, vijiji na mitaa yote katika chaguzi zijazo na
uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba 2015 mwakani.
Alisema Watanzania wanazo rasilimali nyingi katika taifa
hili, kama vile madini na gesi asilia hivyo hawana budi kunufaika navyo na sio
kuendelea kuwa masikini hivyo CCM ambacho ndio chama tawala kinachoongoza
serikali, kina wajibu wa kuhakikisha kwamba wananchi wake wanaboreshewa
miundombinu husika ikiwemo barabara, maji na hata katika sekta ya elimu.
Awali akitoa maelezo kwa viongozi hao wa Mwenyekiti
mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi wilayani Tunduru, ambaye pia ni mkurugenzi
wa siasa na uenezi wa CUF wilayani humo Said Kiosa, alisema katika kuhakikisha
kuwa wanaimwaga CCM, Ukawa wamejipanga
na kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja mmoja kulingana na kila eneo
analokubalika.
Pamoja na mambo mengine, Kiosa alifafanua kuwa makubaliano
ya kufanya hivyo, yalifikiwa Novemba 18
mwaka huu.
No comments:
Post a Comment