Waziri mkuu, Mizengo Pinda. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
BAADHI ya Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma, wanampango wa kwenda kumuona Waziri mkuu wa Jamhuri ya muungano wa
Tanzania, Mizengo Pinda kwa lengo la kufikisha kilio chao juu ya mgogoro ambao
unaendelea kati ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo na Afisa
elimu wa msingi wa wilaya hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi,
Madiwani hao walisema kuwa wamechoshwa na mambo ambayo yanafanywa na mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya Mbinga, Hussein Ngaga kwa kuendekeza migogoro na mambo
yasiyokuwa na tija katika jamii.
Aidha walifafanua kuwa Ngaga ameshindwa kuiongoza wilaya hiyo, kutokana na kuendekeza migogoro na afisa elimu msingi wa wilaya hiyo,
Mathias Mkali na kuchukua hatua ya kumsimamisha kazi kinyume na taratibu za utumishi wa umma wakati hana makosa.
“Hata kama serikali imeunda tume na kuileta hapa kwetu kwa
lengo la kuchunguza mgogoro huu, ni lazima tujipange tukamuone Waziri mkuu,
huyu mkurugenzi hatumtaki kwa sababu hana nia njema ya kutuletea maendeleo sisi
wanambinga, muda mwingi yeye ni mtu wa kupenda kujenga makundi ambayo hayana
maelewano na wenzake”, walisema.
Aidha Madiwani hao walisema wilaya hiyo ambayo sasa
ilionekana kufanya vizuri katika sekta ya elimu msingi, hivi sasa wana wasiwasi
huenda ikashuka kielimu kutokana na mkurugenzi Ngaga kuendeleza malumbano hata
na walimu mashuleni wakiwemo Waratibu elimu kata ambao muda mwingi walikuwa
wakisimamia maendeleo ya watoto mashuleni.
Kufuatia hali hiyo walieleza kwamba, umefika wakati kwa
serikali kuona umuhimu wa kumhamisha mkurugenzi huyo, ili kuweza kunusuru maendeleo
ya wilaya ya Mbinga hususani katika sekta ya elimu ambayo inaonekana sasa
kuanza kuyumba.
“Hivi sasa amefikia hatua ya kuhamisha walimu na waratibu
elimu kata, katika vituo vyao vya kazi na kuwapeleka maeneo mengine, kwa nini
hizi fedha anazotumia kuhamisha hawa watu asifanyie maendeleo mengine ya
wanambinga”? walihoji.
Pamoja na mambo mengine waliongeza kuwa wamefikia mahali
wamechoshwa na matendo yake, hivyo hawaoni sababu ya kuendelea kukaa na
mkurugenzi ambaye muda mwingi anapenda kugombana na watendaji wake wa chini
ambao wanasimamia maendeleo ya wananchi.
No comments:
Post a Comment