Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
BARUA iliyoandikwa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya
wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga juu ya kuifutia usajili asasi ya
Waratibu elimu kata wilayani humo (UWEKAMBI) kwa madai kwamba imeshindwa
kutimiza masharti na taratibu husika, imezua gumzo huku wakisema kuwa
mkurugenzi huyo, amekosa kazi ya kufanya badala yake ajikite katika kufikiria
maendeleo ya wanambinga na sio kuendekeza migogoro ambayo haina tija katika
jamii.
Barua hiyo yenye kumbukumbu namba MDCC/F.10/20/64 ya Novemba
30 mwaka huu ambayo imesainiwa na mkurugenzi huyo, ambapo waratibu hao
walipozungumza kwa nyakati tofauti walisema kuwa kitendo hicho kilichofanywa na
mkurugenzi huyo, si cha kiungwana bali ana mambo yake binafsi ambayo hawatakii
mema wananchi wa wilaya hiyo.
Walisema UWEKAMBI ilianzishwa kwa nia njema na kwa kufuata
taratibu husika za usajili kupitia ofisi yake ya idara ya maendeleo ya jamii,
hivyo yeye anavyosema leo kwamba umoja huo unakiuka sheria, kanuni na taratibu
zinazoongoza misingi ya utendaji kazi wa asasi za kiraia, sio kweli bali
anachuki binafsi huku wakimtaka asitumie vibaya cheo chake alichonacho na
kuingiza mambo binafsi katika utendaji kazi wa maendeleo ya wananchi.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini
kuwa, mkurugenzi Hussein Ngaga ameandika barua hiyo kufuatia mtandao wa
mashirika yasiyokuwa ya kiserikali wilayani Mbinga (MBINGONET) kumpatia taarifa
kupitia barua yenye kumbukumbu namba MBINGONET/MT/MK/068 kuwa, wanampango wa kutembelea
asasi za kiraia na wadau wa elimu kwa baadhi ya kata za wilaya hiyo.
Kufuatia barua hiyo ndiyo iliyoleta uchokonozi na kumfanya
mkurugenzi huyo kuandika barua hiyo, ya kuifutia usajili UWEKAMBI ambayo imekuwa
ikishughulika na masuala ya kukuza kiwango cha taaluma wilayani humo kwa elimu ya
msingi.
Barua hiyo ya kuifutia usajili asasi hiyo, inadaiwa kwamba
ameiandika kwa tarehe hiyo ikionyesha kuwa ni ya siku nyingi, kumbe sivyo na
kwamba kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari vimesema kuwa imeandikwa siku
chache zilizopita, ambapo hata Mwenyekiti wa umoja huo wa waratibu elimu kata
wilayani hapa, Martha Lipa alipoulizwa alisema yeye hajapata barua yoyote
inayotoka kwa mkurugenzi huyo juu ya kuifutia usajili asasi hiyo, bali amekuwa
akisikia maneno mitaani kwamba kuna barua ambayo inasema hivyo.
Mwandishi wa habari hizi ambaye barua hiyo ameipata, yenye
nakala kwenda kwa Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma, Mkuu wa wilaya ya Mbinga na
Mtandao wa asasi za kiraia wilayani hapa (MBINGONET) inathibitisha kwamba
mkurugenzi huyo, ameifutia usajili asasi hiyo ya waratibu elimu kata wa wilaya
hiyo.
Moja kati ya vipengele vya barua hiyo vinasema kuwa “Hivyo
basi, kwa barua hii na kwa mamlaka niliyonayo kisheria na baada ya kujiridhisha
kwa uwepo wa udhaifu katika utendaji wa asasi hiyo ndani ya jamii kinyume na
majukumu yaliyoanishwa hapo juu, natamka rasmi asasi ya UWEKAMBI yenye namba ya
usajili 00CBO/0001 – 768 ambayo imekuwa ikiendeshwa kinyume cha marekebisho ya
sheria ya usajili wa asasi Tanzania, sheria namba 11 (2005) kanuni na taratibu
za usajili 2008 na 2013/2014 za halmashauri ya wilaya ya Mbinga. Hivyo cheti
chake cha usajili ni batili na hakitambuliki ndani ya halmashauri ya wilaya ya
Mbinga”.
Kufuatia hali hiyo nimezungumza na wataalamu wa mambo ya
ushirika kwa nyakati tofauti wilayani humo, wanasema kuwa tendo hilo la
kuifutia usajili asasi hiyo kwa mtindo wa kuiandikia barua bila kukaa kikao na
wadau husika wenye asasi ni ukiukaji wa taratibu na sheria za nchi, hivyo ni batili
na mkurugenzi huyo ameshindwa kufuata taratibu husika ambapo dhahiri inaonesha
kuwa ana nia mbaya na matakwa yake binafsi.
Walisema kama UWEKAMBI alibaini kuna matatizo ni vizuri
angefuata taratibu kuanzia ngazi ya chini kwa kukaa na wahusika, hadi kufikia
maamuzi hayo aliyoyafanya, lakini sio kuchukua hatua ya kukaa mezani na kufanya
hayo aliyoyafanya.
“Hii asasi kama kweli ilisajiliwa kisheria maana yake taarifa
husika za asasi, zipo hadi ngazi ya juu Taifa (RITA) hivyo alipaswa kujenga
hoja zake za msingi za kuifutia kwa kukaa kwanza mezani na wahusika wa asasi,
ndipo kama angebaini kuna tatizo angeweza kuchukua hatua aliyoifanya sasa
lakini sio kufanya mambo kienyeji kama hivi, hiki alichokifanya amejipalia
makaa ya moto yeye mwenyewe huko mbele suala hili litamletea tatizo”, walisema.
Waliongeza kuwa Hussein Ngaga tokea amefika katika wilaya ya
Mbinga, ni mtu wa kupenda kutengeneza migogoro ya hapa na pale kila kukicha
badala ya kufikiria kufanya maendeleo ya wananchi, hivyo ni wakati sasa kwa
serikali kumchukulia hatua za kinidhamu ili iwe fundisho kwake, na watu wengine
wenye tabia kama hiyo.
No comments:
Post a Comment