Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
VIONGOZI
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma, wametakiwa kujenga ushirikiano na
kuacha vitendo vya majungu na fitina ndani ya chama, huku ikielezwa kuwa endapo
kama wataendeleza mambo hayo yatawafanya wagawanyike katika makundi na
kusababisha hata wanachama wa chama hicho wakose imani nao.
Aidha walielezwa kuwa CCM ni chama ambacho kipo madarakani kwa miaka mingi tokea nchi hii ipate uhuru, mikononi mwa Baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere, hivyo wanapaswa kuzingatia taratibu na sheria zilizowekwa kwa mujibu wa katiba husika ili wananchi wasiweze kujengeka na dhana potofu.
Katibu
Mkuu wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM) Sixtus Mapunda alisema hayo wakati
alipokuwa akizungumza na viongozi wa CCM, kwenye ukumbi wa Songea Club uliopo
mjini hapa.
Mapunda alisema “ndugu zangu hiki chama kilianza siku nyingi viongozi tuache tabia hizi, ikiwemo suala la kukaa maofisini na kutaka kuabudiwa badala ya kutekeleza majukumu mliyopewa”.
Alisema
kuwa wanachotakiwa wakae na kujiuliza wametoka na wanakwenda wapi, huku
wakiacha tabia za unafiki, uongo na fitina vitendo ambavyo kama wataviendekeza
havitawafikisha mbali.
“Wewe kiongozi ukibainika unakisaliti chama, tutakushughulikia ipasavyo mpaka Yesu arudi duniani, hatutaki matendo ya hovyo hovyo na kusikia kila kukicha mnagombana”, alisema.
Alifafanua
kuwa Tanzania ni nchi ambayo wananchi wake wanapendana, hivyo chama kilichopo
madarakani hakitakubali kuiacha rehani kwa watu wabovu ambao hawana nia njema
na taifa hili.
Pamoja na mambo mengine aliongeza kuwa nchi haiendeshwi kwa mtindo kama wa kucheza bao, hivyo wameshauriwa kuwa makini na majukumu ya kazi zao za kila siku katika kutumikia wananchi.
Akiwa wilayani Namtumbo:
Katibu huyo wa UVCCM Bw. Mapunda alipokuwa wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, aliwaasa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi wa wilaya hiyo kwamba wawabeze watu ambao wakati wote wamekuwa na tabia ya kupinga maendeleo pale yanapofanyika.
Alisema mifarakano au matatizo yoyote yale yanayojitokeza katika jamii, hayawezi kuleta amani bali hujenga chuki na kuondoa upendo miongoni mwao.
No comments:
Post a Comment