Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa uelewa mdogo kwa viongozi wa serikali na vyama vya
siasa juu ya mipaka ya kazi zao, kumekuwa kukisababisha jamii kukosa haki zao
za msingi na kusababisha wengi wao kuwa maskini.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa kituo cha wasaidizi wa kisheria na
haki za binadamu (WAKIHAMBI) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Daniel
Chindengwike alipokuwa akisoma taarifa fupi ya ufunguzi wa kituo hicho wilayani
humo uliofanyika kwenye ukumbi wa Mbiku hoteli mjini hapa.
Chindengwike alisema kituo hicho kilianzishwa wilayani humo, kwa
lengo la kusaidia jamii katika mambo ya kisheria, ili waweze kupata haki zao
ambazo huporwa na wajanja wachache.
Alisema tokea kituo hicho kianze kufanya kazi zake wilayani
Mbinga, kimeweza kutatua migogoro ya ndoa, ardhi, kesi za madai, usuluhishi na
upatanishi pamoja na matatizo ya ajira kwa watumishi wa serikali ikiwa ni
pamoja na mirathi na viinua mgongo.
Pamoja na mambo mengine, mgeni rasmi katika ufunguzi huo Mkuu wa
wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga alisema jamii inapaswa kutoa ushirikiano kwa
wasaidizi hao wa masuala ya kisheria, ili waweze kutekeleza vyema majukumu ya
kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Ngaga alisema jamii inatakiwa kutambua kuishi katika hali ya
ubinadamu na sio kutendeana mabaya, kwani kufanya hivyo ni dhambi na hata
vitabu vitakatifu vya Mwenyezi Mungu kama vile Bibilia na Korani vinakataza
kufanya matendo mabaya.
Hata hivyo aliongeza kuwa haki na wajibu ndio miongozo ambayo
inaweza jamii kutuongoza duniani, na kutufanya tuwe na maendeleo kwa faida ya
kizazi cha sasa na kijacho.
1 comment:
Msichanganye mambo ya siasa na utendaji WA halmashauri
Post a Comment