Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete. |
Mbinga.
MWANDISHI wa habari Kampuni ya Businesstimes Limited, Kassian
Nyandindi anayeandikia gazeti la Majira wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma,
ameshushiwa kipigo na kutishiwa kuuawa kwa silaha na Afisa usalama wa taifa (DSO)
wa wilaya hiyo (Jina tunalo) katika hoteli ya Gold Farm ya Mbinga mjini.
Habari zilizopatikana mjini hapa, zimeeleza kuwa tukio hilo
lilitokea Novemba 22 mwaka huu, majira ya saa 5 usiku kwenye hoteli hiyo wakati
mwandishi huyo alipokuwa anaaga kurudi nyumbani kwake.
Taarifa zaidi za tukio hilo zilifafanua kuwa, Nyandindi
ambaye alikuwa kwenye ziara ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha
Mapinduzi Taifa (UVCCM) Sixtus Mapunda, alishushiwa kipigo na kigogo huyo wa
usalama wa taifa ambapo baadhi ya wajumbe wa UVCCM wakiwemo maafisa wa umoja
huo toka makao makuu ya chama hicho, walishuhudia tukio hilo.
Aidha wajumbe hao walipoona hali inazidi kuwa mbaya,
walishitushwa na kufikia hatua ya kwenda karibu na tukio hilo na kuingilia kati
ili kuweza kumnusuru mwandishi huyo asiweze kudhurika, licha ya kuwa wakati huo
tayari alikuwa anapigwa mateke na ngumi huku kigogo huyo akiporomosha lugha
chafu akimtukana mwandishi huyo.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida inadaiwa kwamba afisa
usalama huyo wa taifa, baada ya kuona mwandishi Nyandindi amebebwa na kuingizwa
kwenye gari ili apelekwe nyumbani kwake, ghafla alitoka kwenye eneo la tukio na
kwenda kuchukua silaha aina ya bastola, aliyokuwa ameihifadhi kwenye gari lake
ambalo alikuwa ameliegesha nje ya hoteli
hiyo.
Habari zaidi za tukio hilo zilifafanua kuwa wakati silaha
hiyo akiwa ameishika mkononi tayari kwa kutaka kumfyatulia risasi mwandishi wa
habari, baadhi ya wajumbe wa UVCCM waliokuwepo kwenye eneo hilo la tukio
walimdhibiti afisa usalama huyo na kufanikiwa kumnyang’anya silaha hiyo, ambayo
baadae ilidondoka chini na kuokotwa na mmoja wa viongozi hao wa chama huku wakimuuliza
kwa nini unataka kufanya mauaji kwa mwandishi wa habari huyu, ambapo alishindwa
kuwa na majibu zaidi aliendelea kufoka kwa hasira huku akiporomosha matusi.
Katibu mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma,
Benedict Ngwenya alimweleza mwandishi wetu kwamba kitendo alichokifanya DSO
huyo sio cha kiungwana kwa kuwa wameshindwa kuelewa sababu iliyomfanya kutumia
nguvu kubwa kutaka kupoteza maisha ya mwandishi huyo, ambaye alitumia ustaarabu
kuaga kwamba anaondoka anarudi nyumbani, lakini ghafla bila sababu yoyote ya
msingi alijikuta akivamiwa na kigogo huyo.
Vilevile mjumbe wa baraza la umoja huo wa vijana taifa mkoani
humo, Khalfan Kigwenembe alithibitisha kuwa yeye ndiye aliyeiokota silaha hiyo,
na baadae alilazimika kumrudishia baada ya kuona hasira za afisa usalama huyo
zimepungua na mwandishi huyo, tayari alikuwa amepelekwa nyumbani kwake.
Kwa upande wake mwandishi wa habari Nyandindi, alipohojiwa kuhusinana
na tukio hilo alithibitisha kuwa majira hayo ya usiku mara baada ya kuwasili
katika hoteli ya Gold Farm, wakitokea kwenye ziara ya Katibu mkuu wa UVCCM
Sixtus Mapunda, ndipo alikumbwa na tukio hilo.
Nyandindi alifafanua kuwa baada ya kupigwa na kigogo huyo
Novemba 23 mwaka huu majira ya asubuhi, alikwenda Kituo kikuu cha polisi wilaya
ya Mbinga ambako alifanikiwa kufungua jalada la kesi yenye namba
MBI/IR/1978/2014 na kupewa fomu ya matibabu (PF 3) ambayo anaendelea kupatiwa
matibabu.
Alipohojiwa kwa njia ya simu kuhusiana na sakata hilo, afisa
usalama huyo wa taifa wa wilaya ya Mbinga, alikuwa akiongea kwa jazba na kusema
mnauhakika na tukio hili……………. na baadae alikata simu.
Naye Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela
amekiri kutokea kwa tukio hilo, ambalo amedai kuwa tayari limeanza kufanyiwa
kazi.
Hata hivyo Katibu wa Chama Cha Waandishi wa habari mkoani
Ruvuma (RPC) Andrew Chatwanga alisema, taarifa za kupigwa mwandishi wa habari
Nyandindi amezipokea na kwamba tayari ameitisha kamati ya utendaji ya chama
hicho, kwa lengo la kutaka kutoa tamko dhidi ya afisa usalama huyo ambaye
alimshambulia mwandishi huyo kwa kumtishia kutaka kumuua kwa silaha.
No comments:
Post a Comment