Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.
WANAFUNZI wanaosoma katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii (FDC)
wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameandamana kwenda katika ofisi ya Mkurugenzi
mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, kutokana na choo wanachokitumia kujaa
na kusababisha harufu kali katika eneo la chuo hicho.
Tukio hilo lilitokea Novemba 3 mwaka huu majira ya asubuhi,
ambapo walieleza kwa nyakati tofauti kuwa walifikia hatua ya kufanya hivyo
kutokana na uongozi husika wa chuo hicho, kutochukua hatua za haraka katika
kunusuru hali hiyo.
Walisema baada ya kuona tatizo hilo halifanyiwi kazi kwa muda
mrefu, waliona ni vyema wapeleke kilio chao kwa Mkurugenzi mtendaji wa wilaya
ya Mbinga Hussein Ngaga, ili tatizo hilo la choo kufurika lifanyiwe kazi
haraka.
Aidha walipofika katika eneo la ofisi za Mkurugenzi huyo,
wanafunzi hao walielezwa kwamba wasiwe na jazba hivyo warejee katika eneo la
chuo ambapo baada ya kufanya hivyo, baadhi ya viongozi wa kata ya Mbinga mjini
akiwemo Ofisa tarafa wa Mbinga mjini, walikwenda huko kuzungumza na wanafunzi
hao na uongozi wa chuo cha FDC ili kuweza kumaliza kero hiyo.
Akihojiwa na waandishi wa habari, Mkuu wa chuo hicho cha
maendeleo ya jamii wilayani hapa Aidan Mchawa alisema hasira za wanachuo hao kuandamana
zilitokana na uongozi husika wa chuo, kuchelewa kufanyia matengenezo ya choo hicho
ambacho kimejaa.
Mchawa alisema tatizo hilo la kuchelewa lilitokana na chuo
kukosa fedha za kuweza kufanya kazi hiyo, hivyo jitihada zitafanyika za kuweza
kumaliza kero hiyo mapema iwezekanavyo.
“Chuo hiki kina wanafunzi 150 wote hawa waliandamana kupinga
tatizo hili ambalo lipo mbele yetu, tulijaribu kuwatuliza wasifanye hivi lakini
ilishindikana kutokana na wengi wao kuwa na hasira kali”, alisema Mchawa.
No comments:
Post a Comment