Rais Jakaya Kikwete, wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
OFISI
ya Mkaguzi wa ndani Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imeshushiwa
shutuma nzito kwamba inashindwa kutekeleza majukumu yake ya kazi kwa mujibu wa
taratibu na sheria zilizowekwa, badala yake inatoa taarifa zenye mapungufu na
kuleta migogoro isiyokuwa na tija, mtandao huu umeambiwa.
Mkaguzi wa ndani wa halmashauri hiyo
Laston Kilembe, ndiye anayeshushiwa shutuma hizo na baadhi ya madiwani wa
wilaya hiyo, walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati
tofauti.
Walisema
hata Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, alimuagiza mkaguzi huyo katika
kikao cha baraza la madiwani kilichoketi Julai 26 mwaka huu mjini hapa, kwamba
ahakikishe anatoa taarifa sahihi na kwa wakati ili kuepukana na malalamiko yasiyokuwa
ya lazima.
Sambamba
na hilo Mkuu huyo wa mkoa aliwataka hata watendaji wa serikali katika
halmashauri hiyo, kutoingilia utendaji kazi wa ofisi ya mkaguzi huyo huku
akisema kuwa ni ofisi ambayo ipo huru na inafanya kazi zake bila kuingiliwa na
mtu yeyote.
Walifafanua
kuwa ofisi ya mkaguzi wa ndani katika halmashauri yoyote hapa nchini, ni idara
kamilifu ambayo ipo huru na haipaswi kuingiliwa na mtu.
Walibainisha
mambo hayo yote yanatokana na madiwani kupinga taarifa yake ya ukaguzi kwamba
ina mapungufu, juu ya tuhuma anazotuhumiwa Afisa elimu msingi wa wilaya ya
Mbinga kwamba ni mwizi wa mafuta na fedha za michango ya wananchi.
Diwani
wa kata ya Litembo Altho Hyera alisema anamshangaa Bw. Kilembe
kuwasilisha tuhuma hizo kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichoketi
hivi karibuni, huku akijua fika taarifa yake haikukamilika na ina mapungufu
makubwa kutokana na kufanya ukaguzi usiokidhi matakwa husika.
Hyera
alisema taarifa hiyo ambayo madiwani waligawiwa katika kikao hicho alipomaliza
kuisoma mbele ya baraza, ghafla walishangaa kumuona Mkurugenzi mtendaji wa
halmashauri hiyo Hussein Ngaga anasimama na kusema taarifa hiyo bado
haijakamilika inafanyiwa kazi itatolewa majibu katika kikao kingine kijacho cha
madiwani.
Alisema
baadae Mkurugenzi huyo aliamrisha taarifa zote zilizokuwa mikononi mwa madiwani
zikusanywe watapewa tena katika kikao kijacho, jambo ambalo wengi wao walikuwa
wakihoji kama taarifa hiyo ilikuwa na mapungufu na haijakamilika kwa nini
ililetwa mbele ya baraza hilo na kuwasilishwa?.
Kufuatia
hali hiyo ndipo walipoelekeza hasira zao kwa mkaguzi wa ndani kwamba anashindwa
kutekeleza majukumu yake ya kazi ipasavyo, badala yake anatengeneza majungu
yenye kuleta mifarakano kati ya madiwani na watendaji wa serikali katika
halmashauri hiyo.
Waandishi
wa habari walipokwenda ofisini kwa mkaguzi wa ndani wa halmashauri ya wilaya ya
Mbinga Laston Kilembe, kumtaka atolee ufafanuzi juu ya malalamiko hayo alikataa
kuzungumzia lolote huku akisema mpaka apate kibali kutoka kwa mkurugenzi wake.
“Siwezi
kuzungumza nanyi mpaka mpate kibali kutoka kwa mkurugenzi, fuateni taratibu
mkurugenzi mimi ni bosi wangu, hata kama ofisi yangu inafanya kazi zake bila kuingiliwa
na mtu yoyote lakini siwezi kuzungumza lolote mpaka nipate kibali kutoka
kwake”, alisema Kilembe.
No comments:
Post a Comment