Na Willy Sumia,
Sumbawanga.
WATU
wawili wamefariki dunia kutokana na kulewa pombe na kuwa
chakari wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa, kitendo ambacho kiliwasababishia kuzama
katika mto wakati walipokuwa wakirejea nyumbani.
Kitendo
cha kuzama mtoni, watu hao wanadaiwa kupoteza maisha baada ya kushindwa kuvuka
mto walipokuwa wakirejea kutoka kunywa pombe nyakati za usiku katika tarafa ya
Mtowisa wilayani humo.
Waliopoteza
maisha wametajwa kuwa ni Leonard Salehe (44) mkazi wa kijiji cha Zimba na
Gilbert Machimu (47) mkazi wa kijiji cha Sakalilo.
Imeelezwa
kuwa hivi karibuni, Leonard Salehe alikuwa ametoka matembezini akiwa amelewa na
alipofika katika mto Mkanga alishindwa kujimudu na kuyumba hadi kwenye mkondo
wa maji na kuzama hadi alipokutwa na umauti.
Gilbert
Machimu alikuwa ametoka matembezini naye akiwa amelewa pombe za kienyeji
alipofika katika mto Zimba, alishindwa kujimudu na kuyumba hadi mtoni ambako
maji yalimzidi nguvu na kufariki dunia.
Kamanda
wa polisi mkoani Rukwa, Jacob Mwaruanda alisema uchunguzi wa awali ulibaini
kuwa vifo vyote hivyo vilisababishwa na ulevi uliopindukia, ambao uliwafanya marehemu
hao kushindwa kujimudu na kuzama katika maji ya mito hiyo, walipokuwa wakirejea
majumbani kwao.
Msimu
wa kiangazi katika mkoa huo, huwa kunaibuka tabia ya kunywa pombe kupita kiasi
kutokana na kukamilika kwa mavuno na kuongezeka kwa kipato baada ya kuuza mazao
yao hasa mahindi.
No comments:
Post a Comment