Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
JINAMIZI linalodaiwa kutengenezwa na Mkurugenzi mtendaji wa
Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga katika kuhakikisha
linaendelea kumsakama Afisa elimu msingi Mathias Mkali na walimu wake, imeelezwa
kuwa ni dalili tosha zinazoashiria kurudisha nyuma maendeleo katika sekta ya
elimu msingi wilayani humo, ambapo hivi sasa limeingia katika sura mpya kwa
walimu wakuu wa shule hizo likitaka taarifa ya mapato na matumizi ya fedha za
TSM. 9 na Capitation zinazopelekwa mashuleni.
Mkurugenzi huyo amewaandikia barua walimu hao ambayo nakala
yake tunayo, yenye kumbukumbu namba MDCC/F. 10/20/43 ya Novemba 10 mwaka huu, ikiwataka
waandae taarifa hiyo ya kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2011 hadi sasa
2014/2015.
Baadhi ya walimu waliokuwa wakizungumza na mwandishi wa
habari hizi kwa nyakati tofauti walisema, wanamshangaa Mkurugenzi huyo
kuwaandikia barua hiyo ambayo ameichelewesha kuwafikia walimu hao, ikiwataka kufanya
kazi hiyo jambo ambalo ni vigumu huku wengine wakibeza
na kusema huenda anatafuta sababu kwa mwalimu atakayekosea na kushindwa
kukamilisha kwa wakati apate cha kusemea.
Walisema wamechoshwa na mambo yake tokea aingie katika wilaya
ya Mbinga, amekuwa ni mtu wa kuongoza wenzake kwa njia ya migogoro na kuwatafutia
sababu zisizo na msingi badala ya kukaa na kubuni mipango ya kimaendeleo, huku
wakiongeza kuwa kazi hiyo ilibidi aikamilishe Mkaguzi wake wa ndani, Laston
Kilembe alipokuwa akipita hivi karibuni kuhoji mashuleni kwa walimu wakati
anafanya ukaguzi wake juu ya fedha hizo, lakini mkaguzi huyo hakufanya hivyo
ndio maana hivi sasa walimu hao wanasumbuliwa akiwataka watekeleze hilo.
“Kitendo cha Mkurugenzi huyu kutaka taarifa hizi za mapato na
matumizi kwa kutupeleka kwa uharaka wa siku chache namna hii, sio taratibu
nzuri tukiwa sisi watumishi wa serikali kama alivyo yeye”, walisema.
Uchunguzi uliofanywa na mtandao huu umebaini kuwa hayo yote
yanajitokeza baada ya Hussein Ngaga kumsimamisha kazi Afisa elimu msingi
Mathias Mkali akisema kuwa ni mwizi wa fedha za serikali na michango husika ya
wananchi, huku wazazi, walimu na wananchi wa wilaya ya Mbinga wakipata taharuki
na mshangao juu ya mambo anayoyafanya mkurugenzi huyo dhidi ya mtumishi
mwenzake.
Kadhalika wazazi na wananchi kwa ujumla wanahoji kwamba,
endapo kama Afisa elimu huyo ni mwizi, inakuwaje ameweza kufanikisha utendaji
wa kazi zake kwa kufaulisha vizuri watoto wao tokea alipohamia Mbinga, kupitia michango
yao waliyokuwa wakichanga na ile inayotolewa na shule kwa ajili ya mitihani ya kila
mwezi kwa wanafunzi?
Tafiti zinaeleza kuwa Mkurugenzi huyo katika barua yake
aliyowaandikia walimu wakuu mashuleni ambazo walimu hao wanalalamika zimechelewa
kuwafikia, na kuwataka wawasilishe taarifa hiyo Novemba 19 mwaka huu wanatakiwa
kuandaa na kuwasilisha taarifa ya mapato na matumizi ya fedha, walizopokea
kutoka kwa wananchi (Wazazi) na Halmashauri ya wilaya hiyo kwa mwaka wa fedha
wa 2011 hadi 2014/ 2015.
Barua hiyo inasema anawataka wawasilishe taarifa ya; michango
ya fedha za TSM. 9, michango ya fedha za mitihani, fedha za Capitation,
ongezeko la fedha za mitihani darasa la saba kwa mwaka 2014 pamoja na fedha
zingine tofauti na zilizotajwa katika barua yake aliyowaandikia walimu hao kitendo
ambacho kinawashangaza walimu hao wakisema, kazi hiyo ilibidi aikamilishe Mkaguzi
wake wa ndani wa halmashauri hiyo pale alipomtuma hivi karibuni apite mashuleni
kufanya ukaguzi.
Aidha Ngaga katika barua yake amewataka walimu hao katika
taarifa zao waonyeshe fedha zote zilizopokelewa na shule, na baadaye kuhamishiwa
kwenye akaunti ya Umoja Waratibu Elimu Kata Wilaya ya Mbinga (UWEKAMBI) huku
akijua fika fedha zinazopelekwa kwenye umoja huo ni mpango ambao ulibarikiwa
katika vikao halali vya halmashauri hiyo, ikiwemo baraza la madiwani na kamati
za shule mashuleni.
Vilevile pamoja na maagizo hayo Mkurugenzi huyo amewapa barua
za kuwataka pia watendaji wa kata kufuatilia suala hilo, huku wengi wao wakilalamika
wakisema kazi hiyo ni jukumu la Waratibu elimu kata, kamati za shule na walimu
wake hivyo wao ni sawa na kuwatwisha mzigo wa kazi ambayo sio jukumu lao.
Mwandishi wa habari hizi baada ya kufuatilia sera, sheria na
kanuni za Wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi namba 25 ya mwaka 1978 na
marekebisho yake ya mwaka 1995 inatamka wazi kuwa jukumu hilo ni la kamati za
shule, mashuleni yenye mamlaka ya kuidhinisha matumizi ya fedha za shule na
kuitisha vikao vya wazazi, walezi na jamii pale inapotakiwa kutoa taarifa
husika na sio kuwatuma watendaji wa kata kusimamia zoezi hili, hivyo kufanya
hivyo ni kukiuka miongozo ya wizara.
Pamoja na mambo mengine Mkurugenzi wa halmashauri ya Mbinga
Hussein Ngaga alipotafutwa ili aweze kuzungumzia suala hilo hakuweza kupatikana
hadi pale habari hizi zilipokuwa zinaingia mitamboni.
No comments:
Post a Comment