Katibu Mkuu UVCCM Taifa, Sixtus Mapunda akiwasili katika ofisi kuu ya CCM wilayani Mbinga. |
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM) Sixtus Mapunda akizungumza na wananchi wa kata ya Mpepai wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma. |
Mbinga.
KATIBU wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM) Sixtus Mapunda
amesema, serikali nchini ipo tayari kumchukulia hatua za kinidhamu kiongozi
yeyote aliyekuwa madarakani, ambaye anaonesha kuwa na matendo ya hovyo kwa
wananchi wake na yenye kurudisha nyuma
maendeleo husika.
“Ndugu zangu wananchi hatupo tayari mahali popote pale, kumvumilia
Mkuu wa wilaya au Mkurugenzi mtendaji mwenye matendo ya hovyo na yenye
kukatisha tama wananchi, tukisikia tunamwondoa haraka tunahitaji kiongozi
mwenye kujali maisha na maendeleo ya watu wake”, alisema.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu huyo leo, alipokuwa akihutubia
wananchi wa kata ya Mpepai wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kwenye mkutano wa
hadhara, uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Mpepai wilayani humo.
Mapunda alisema kuwa itakuwa ni ajabu kwa chama tawala, Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kumkalia kimya bila kumwajibisha kiongozi ambaye hana nia
njema na taifa hili, huku akiwaacha wananchi wakiteseka kutokana na mambo yake
binafsi ambayo hayana tija katika jamii.
Pamoja na mambo mengine, Mapunda alizungumzia tatizo la
mlundikano wa mahindi yaliyopo hapa wilayani Mbinga, ambayo serikali haija ya
nunua, hivyo alieleza kuwa atakwenda kuzungumza na Rais Jakaya Kikwete ili
kuona namna ya kunusuru hali hiyo.
Aliongeza kuwa wilaya hiyo hivi sasa ina mahindi mengi, ambapo
inahitajika nguvu ya ziada kuona namna gani yananunuliwa ili wakulima waweze
kupata hata fedha za kuendeshea maisha yao, ikiwemo kupeleka watoto wao shule.
Vilevile alifafanua kwamba atakapokutana na Rais Kikwete, atamuomba
wazungumze na balozi wa nchi ya Kenya ambaye yupo hapa nchini, ili mahindi hayo
yanunuliwe na kusafirishwa mpaka huko, kutokana na nchi hiyo hivi sasa inakabiliwa
na tatizo la njaa.
“Tunachangamoto kubwa ya mlundikano wa mahindi hapa Mbinga,
taarifa ninazo lakini napenda kuwaambia tutaona namna ya kumaliza kero hii, ili
ndugu zangu wakulima nanyi muweze kupata fedha za kusukuma mbele maendeleo yenu”,
alisema Mapunda.
Kadhalika alifafanua kuwa serikali itaendelea kufanya
jitihada ya kutatua matatizo ya wananchi, hivyo amewataka waendelee kuwa na
moyo wa kushiriki kikamilifu katika kuendeleza kauli mbiu ya kilimo kwanza ili
taifa lisipatwe na baa la njaa.
Katibu wa UVCCM taifa, Bw. Mapunda yupo katika ziara
yake ya kikazi ya siku tatu hapa mkoani Ruvuma.
No comments:
Post a Comment