Friday, November 14, 2014

GAUDENCE KAYOMBO: KATIKA HILI MKURUGENZI WAKO WA MBINGA AMEKENGEUKA

Gaudence Kayombo, Mbunge wa Jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma. 
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

SIRI imefichuka juu ya mgogoro ambao unaendelea kufukuta, kati ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, na Afisa wake wa elimu ya msingi Mathias Mkali kwamba baadhi ya Madiwani wa kata ya Mkako na Mkumbi wilayani humo ndio wanaohusika kwa kiasi kikubwa kuuendeleza mgogoro huo, ambao sasa unahatarisha kurudisha nyuma maendeleo katika sekta ya elimu msingi wilayani humo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi, baadhi ya Madiwani wa wilaya hiyo walimtaja diwani wa kata ya Mkako Ambrose Nchimbi na Bruno Kapinga kutoka Mkumbi, ndio wanaohusika kwa karibu zaidi katika kuufanya mgogoro huu uendelee kufukuta na baadhi ya watendaji wa serikali kujengeana chuki.

Walisema kitendo hicho wanachokifanya Madiwani hao kwa kushirikiana na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Hussein Ngaga kutaka kumng’oa Afisa elimu msingi wa wilaya ya Mbinga, wamekuwa wakitengeneza mambo yasiyokuwa na ukweli na ni dhambi ambayo itakuja kuwatafuna baadae.

Aidha walieleza kuwa kitendo cha Nchimbi na Kapinga kujiingiza katika mgogoro huu, ni sawa na kuwasaliti madiwani wenzao na wananchi wa Mbinga kwa ujumla hivyo wanachotakiwa waachane na mambo hayo badala yake, wajikite katika kupigania maendeleo ya wanambinga na sio kuendekeza mambo ambayo hayana manufaa kwa jamii.

Awali ya yote chanzo cha mgogoro huo ni kwamba Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Hussein Ngaga amemtengenezea Bw. Mkali tuhuma kadhaa ikiwemo kuwa Afisa elimu huyo ameunda NGO inayofahamika kwa jina la (UWEKAMBI) na kutumia fedha za Capitation, michango ya wananchi na TSM 9 ambazo zote ni fedha za serikali bila idhini ya miamala husika ambapo ukweli ni kwamba umoja huo, uliundwa kisheria kupitia ofisi ya Mkurugenzi huyo Aprili 24 mwaka 2012 na kupewa baraka katika vikao vya baraza la madiwani.


Hivyo sio kitu kigeni kiasi cha kukijengea tuhuma kwa uwepo wake na kazi zake kwani, ni umoja ambao unafahamika na walimu wote wakiwemo walimu wakuu, madiwani na hata uongozi wa wilaya hiyo.

Uchunguzi umebaini kuwa katika umoja huo Afisa elimu huyo ambaye anatuhumiwa, sio mwanachama na mtia saini kiasi cha kufikia kutuhumiwa bali yeye kwa cheo chake ni mlezi wa umoja huo.

Vilevile mamlaka husika zinazoidhinisha matumizi ya fedha za wananchi na Capitation kadri ya mwongozo wa MMEM unavyosema, ni kamati za shule na kwa upande wa wilaya ni baraza la madiwani ambapo kamati za shule hufanya kazi yake kwa kufuata mwongozo huo wa MMEM kwa mfano matumizi ya fedha za Capitation wanazingatia mwongozo wa mgawanyo kwa vifungu kama ifuatavyo;

  • Mitihani asilimia 20
  •  Utawala asilimia 20
  •  Ukarabati asilimia 30 na
  • Vifaa asilimia 30

Uchunguzi zaidi umebaini kuwa idhini ya kukusanya michango ya fedha za mitihani toka mashuleni na kupeleka mfuko wa akaunti ya UWEKAMBI ilitolewa na mamlaka husika ambapo ni; kikao cha walimu wakuu wote kilichofanyika Januari 12 mwaka 2013 kwa niaba ya kamati za shule ambacho kiliridhia na kukubaliana fedha za mitihani ngazi ya kata zihifadhiwe na umoja huo, badala ya kila mratibu kuhifadhi mwenyewe mfukoni mwake.

Hata hivyo kikao cha madiwani cha kamati ya Elimu, Afya na Maji kilichofanyika Aprili 1 mwaka huu na kikao cha baraza la madiwani cha Aprili 25 mwaka huu kiliridhia, uendeshaji wa mitihani kwa kutumia akaunti husika ya pamoja ya waratibu elimu kata (UWEKAMBI) ina kibali cha mamlaka husika kadri ya mwongozo wa MMEM 2002 hadi 2006.

Chakushangaza imebainika kuwa Mkaguzi wa ndani Laston Kilembe, pamoja na kwenda mashuleni kufanya ukaguzi lakini alishindwa kabisa kufika ofisi ya umoja huo wa waratibu elimu kata iliyopo mjini hapa, ambao unahusika kupokea michango ya fedha za mitihani ya watoto mashuleni kwa lengo la kukagua mapato na matumizi badala yake alifanya ukaguzi wake kwa kutumia Bank Statement (NMB) ya UWEKAMBI na kutoa tuhuma za wizi wa fedha za michango ya wananchi na Capitation.

Kwa mtazamo wa kawaida inaonesha kwamba ukaguzi huo ulikuwa elekezi kutoka kwa kigogo mmoja wa ngazi ya juu wa Halmashauri ya Mbinga Hussein Ngaga, kwani ulilenga kukagua bank statement pekee bila kutaka kujua mapato na matumizi na hata huko mashuleni hakukagua vitabu vinavyohusika na mambo ya fedha, badala yake walimu waliulizwa maswali tu pasipo kupitia vitabu vya fedha kitu ambacho ni kinyume na taratibu za ukaguzi.

Katika hili kwa mtazamo wangu, wakati umefika kwa serikali kuwa makini na wakaguzi aina ya Bw. Kilembe kwani anatia shaka juu ya ukaguzi wake na kwamba kama ataendelea na hali hiyo ya kupokea maelekezo kutoka kwa watu ambao hawana taaluma hiyo, ni hatari kwani huenda akasababisha maendeleo yanayokusudiwa kuelekezwa miongoni mwa jamii kushindwa kupatikana.

Tuhuma zingine ambazo zinaonesha kuleta mashaka dhidi ya Afisa elimu huyo ambazo Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Hussein Ngaga anazituhumu, wasomaji wetu endeleeni kufuatilia mtandao huu ili muweze kufahamu ukweli kuhusu sakata hili.........................................

Pamoja na mambo mengine kufuatia hali hiyo kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, kwa kushirikiana na Mbunge wa jimbo la Mbinga Gaudence Kayombo, hivi karibuni ilifanya kikao cha dharula kinachodaiwa kuitishwa kwa shinikizo la Mbunge huyo kwa lengo la  kujadili mambo hayo ambayo yanaonekana kuipeleka wilaya kubaya hususani katika sekta ya elimu msingi.

Licha ya suala hilo, siri imeibuka kutoka kwenye kikao hicho kuwa Mbunge huyo na Mkuu wake wa  wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga walikuwa ndani ya kamati hiyo, wakishusha lawama na kuhoji kuwa kwa nini Chama hicho ngazi ya mkoa kilipanga kufanya kikao cha Halmashauri kuu ya mkoa wilayani Mbinga Novemba 9 mwaka huu, Kwa nini Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya mkoa Oddo Mwisho alipofungua kikao hicho alisema matatizo ya Mbinga na aliyapata wapi? na mwisho walihoji Mabango yaliyotolewa mbele ya Waziri wa ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Dokta Hussein Mwinyi aliyaandika nani?

Vilevile mtandao huu ulifanikiwa kufanya mahojiano na Mbunge Kayombo, ambapo alionekana kuwatetea vigogo wa wilaya hiyo kwa kuunga mkono kwamba ofisa elimu msingi Bw. Mkali ndiye mwenye makosa.

Alisema watu wa Mbinga watulie, huku tuhuma za Afisa elimu huyo zinafanyiwa kazi badala yake waache mchakato, taratibu na kanuni husika zinaendelea kufuatwa na majibu yatatolewa baadae katika baraza la madiwani kwa maamuzi zaidi.

“Ifike mahali ili tuweze kujua huyu mtu ana makosa au hana makosa ni vyema tukae kimya na sio kuendelea kulikuza jambo hili kuwa kubwa”, alisema Kayombo.

Kwa upande wa Mkuu wa wilaya ya Mbinga imeelezwa kuwa alipaswa kulimaliza tatizo hilo mapema, kwa kuzikutanisha pande zote mbili badala ya kuegemea upande mmoja wa shilingi huku upande mwingine ukizidi kudidimizwa, jambo ambalo ni kinyume cha haki za binadamu na sheria za kiutumishi kwa ujumla.

Senyi Ngaga alipotafutwa ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya sakata hili, hakuweza kupatikana na mtandao huu utaendelea kumtafuta ili aweze kuzungumzia jambo hilo.



No comments: