Waziri wa ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, Hussein Mwinyi akisalimiana na wana CCM wakati alipowasili katika ofisi za makao makuu ya chama hicho wilayani Mbinga. |
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho akisistiza jambo ndani ya kikao cha Halmashauri kuu ya mkoa wa Ruvuma kilichofanyika ukumbi wa Jumba la maendeleo wilayani Mbinga. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida Waziri wa ulinzi na Jeshi la
kujenga Taifa (JKT) Dokta Hussein Mwinyi, ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) taifa,
amepokelewa kwa mabango wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, yakiwatuhumu baadhi ya
vigogo wa ngazi ya juu wilayani humo kufuatia mgogoro mkubwa uliopo kati ya
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri na Afisa elimu wa shule za msingi wa wilaya
hiyo.
Baadhi ya wananchi ambao ni wanachama wa CCM, ndio
walioshika mabango hayo ambayo yalikuwa na ujumbe uliosomeka kuwa; Afisa elimu wetu anaonewa, Mkurugenzi wa
halmashauri hatumtaki ondoka nae, Afisa usalama wa taifa (DSO) hatufai ondoka
nae, Hawa ndio wanaoimaliza CCM Mbinga, Wananchi wanaichukia CCM kupitia hawa
watu na mwishoni kabisa yalikuwa yakimalizia kwa kauli ya Tafadhali sikiliza
vilio vyetu wanambinga.
Hayo yote yalitokea wakati Waziri Mwinyi anawasili katika
viwanja vya makao makuu ya Ofisi za Chama cha mapinduzi wilayani Mbinga, leo
majira ya saa 5: 30 ambapo wanachama hao walionekana kujawa jazba huku wakipinga
mgogoro huo ambao unaendelea kufukuta mpaka sasa wilayani humo.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wanachama hao ambao walionekana
wameshika mabango hayo ambayo yalisheheni ujumbe huo wa kuwakataa viongozi hao wa
wilaya hiyo, ghafla alijitokeza Mkuu wa wilaya ya Songea mkoani hapa Joseph
Mkirikiti ambaye alimwakilisha Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, akiwa
ameongozana na Afisa usalama wa taifa wa wilaya ya Mbinga (Jina tunalo)
walikwenda mbele ya mabango hayo na kuyanyang’anya na baadae wanachama hao
walikamatwa na kufikishwa kituo kikuu cha Polisi cha wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotufikia, zinaarifu
kuwa wanachama hao walikuwa wakihojiwa na kuchukuliwa maelezo kituoni hapo na
kuambiwa kesho Novemba 10 mwaka huu majira ya saa 2:00 asubuhi wakaripoti tena.
Aidha wanachama hao wanatuhumiwa kuwa ndio waliohusika
kusambaza waraka uliosheheni tuhuma mbalimbali, ambazo zinamtuhumu Mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Hussein Ngaga kuwa anamuonea Afisa
elimu wa shule za msingi wilayani humo Daud Mathias Mkali.
Waziri akabidhiwa
waraka wenye taarifa ya kusimamishwa kazi Afisa elimu msingi wilaya Mbinga:
Wakati Waziri Mwinyi anawasili katika viwanja vya Chama cha
mapinduzi wilaya ya Mbinga, baadhi ya wanachama wa chama hicho Monica Msuku na
Salima Mkeso walimkabidhi taarifa ya maandishi juu ya kusimamishwa kazi Afisa
elimu wa wilaya hiyo Bw. Mkali ambayo nakala yake tunayo, ambapo imefafanua
dhahiri kuwa afisa elimu huyo anaonewa.
Moja kati ya sehemu ya taarifa hiyo ambayo inakurasa nane, inaeleza
kuwa tuhuma anazotuhumiwa afisa elimu huyo, mazingira ya vikao vyote
vilivyoshughulikiwa dhidi yake na mwisho kwenye kikao cha baraza la madiwani
cha tarehe Oktoba 27 mwaka huu yaliandaliwa na kutumika kama njia na silaha
pekee ya kumuazimia, kumwajibisha na kumchukulia hatua zaidi, sambamba na
madiwani kumkataa.
Vilevile Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo,
katika kipindi chote cha mwaka mmoja alichofanya naye kazi Afisa elimu huyo,
hajawahi kuitwa au kuonya kuhusiana na masuala ya kazi, hata pamoja na
kutokuonya na kufanya kazi kwa bidii na uadilifu amekuwa akikumbana na
changamoto zinazohusiana na mambo ya fedha, ambayo ameyafanya Mkurugenzi wa
wilaya ya Mbinga kama ifuatavyo;
Na nukuu;
Mkurugenzi mtendaji katika taarifa hiyo anadaiwa, kupunguza
bakaa la fedha za idara ya elimu msingi, ambapo wakati wa Juni 30 mwaka 2013
idara hiyo ilibakiwa na fedha shilingi milioni 127,110,696.90 lakini siku
iliyofuata Julai 1 mwaka 2013 aliigawia idara ya elimu msingi bakaa la shilingi
milioni 73,000,000. Afisa elimu msingi alipojaribu kufuatilia kwa kuwasiliana
na Mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo alikuwa mkali na kumfokea.
Jambo lingine ni kwamba Mkurugenzi huyo anadaiwa, kutopeleka
fedha za Capitation kwa wakati kadri ya miongozo ya MMEM na fedha kukaa zaidi
ya mwaka bila kupelekwa mashuleni, na alipojaribu Afisa elimu kuandika barua za
kukumbusha ili kusisitiza fedha ziende kwa wakati pia alifokewa na kujengewa
uadui ambao unaendelea hadi sasa.
Aidha fedha za Capitation za mwaka 2012/2013 jumla ya
shilingi milioni 54,725,000 hazijapelekwa shuleni mpaka sasa, pamoja na
Wakaguzi wa mkoa kukagua na kutoa hoja hiyo Novemba 11 mwaka 2013 pamoja na
kikao cha kamati ya mipango na fedha cha Julai 10 mwaka huu kupitia hoja hiyo
na kuweka msisitizo, pamoja na msisitizo wa kikao cha Mhe. Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania cha Marchi 1 mwaka huu lakini hadi Oktoba 16 mwaka huu
fedha hizo za Capitation zilikuwa hazijapelekwa mashuleni.
Idara iliandaa fedha za kuwalipa walimu waliofundisha muda wa
ziada wakati wa likizo ya Desemba 2013 lakini fedha hizo, baada ya kutoka
zilichukuliwa na Mkurugenzi mtendaji wa wilaya kwa maelezo ya kuwa anaziazima
lakini hadi leo hii walimu hawajalipwa.
Kipindi cha mwezi Juni 2014 Afisa elimu aliitwa nyumbani
kwake Mkurugenzi mtendaji wa wilaya ya Mbinga, na kuagizwa awasiliane na
uongozi wa Waratibu elimu kata wampatie fedha shilingi milioni 10,000,000
kutoka katika mfuko wa umoja wa waratibu hao (UWEKAMBI), agizo ambalo afisa
elimu alishindwa kulitekeleza na badala yake kujengea uhasama uliopelekea
kuanza kuwasakama waratibu elimu kata, na kumhusisha afisa elimu kama kiongozi
wa idara na kudai kuwa huo umoja wa kazi wa waratibu elimu kata ni NGO yake.
Idara ya elimu ya msingi kwa muda mrefu maombi na madokezo ya
fedha yalikuwa hayapitishwi na kuidhinishwa kwa malipo, hali iliyosababisha
hata gari la idara hiyo kufanyiwa matengenezo kwa fedha za mfukoni ikiwa pamoja
na kununua matairi na betri.
Mwisho wa taarifa hiyo unaeleza kuwa hali hiyo imedumu mpaka
siku Afisa elimu msingi anasimamishwa kazi, ndipo Mkurugenzi mtendaji wa wilaya
ya Mbinga alikwenda idara ya elimu kuwataka walete madokezo yao yapitishwe na
yalipitishwa kwa siku moja.
Yaliyojiri katika
kikao:
Pamoja na mambo mengine Waziri Mwinyi ambaye pia ni mlezi wa CCM
mkoa wa Ruvuma, wakati anawasili katika kikao alichoandaliwa kwenye ukumbi wa
Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa, ili aweze kuzungumza na wajumbe wa
Halmashauri kuu ya mkoa huo, mapya yaliibuka katika mkutano huo ambapo
Mwenyekiti wa chama hicho mkoani hapa Oddo Mwisho ndiye aliyeibua hasira kutoka
kwa wanachama wengine, juu ya mgogoro
huo unaoendelea kufukuta kati ya afisa huyo wa elimu msingi na mkurugenzi wake
mtendaji huku akimtaka Waziri huyo kuingilia kati ili kuweza kunusuru maendeleo
ya elimu wilayani humo.
“Suala hili la mgogoro kati ya mkurugenzi huyu na afisa
elimu, mimi nasema endapo kama litaendelea nipo tayari kulifikisha kwa viongozi
wa ngazi ya juu ili lifanyiwe kazi, hatutaweza kuvumilia migogoro ya watendaji
wa serikali inaendelea katika wilaya hii, hapa anayeumia ni mwananchi wa
kawaida”, alisema Mwisho.
Mwenyekiti wa CCM
wilaya Mbinga awa Mbogo:
Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wilaya ya Mbinga Christantus
Mbunda, aligeuka kuwa mbogo katika kikao hicho huku akiwanyoshea kidole
viongozi wa ngazi ya juu wa wilaya hiyo,
akisema kwamba ndio wanaolea na kushabikia mgogoro huo uendelee kukua huku wakiendelea
kukaa maofisini bila kuchukua hatua madhubuti.
Mbunda alisema ofisini kwake ameletewa barua nyingi za
malalamiko juu ya tatizo hilo, lakini akiwa katika vikao husika na viongozi
wenzake wa wilaya hiyo wanaonekana wakimpinga na kutoonesha njia ya kufanya
utatuzi.
Alisema kwamba, ili kuweza kufanikisha suala hilo liweze kufikia
hatua ya kwisha kwa amani ni vyema ngazi ya chama mkoa na taifa kwa ujumla,
wakaingilia kati ikiwemo hata kuwajibisha watendaji ambao wanaonekana kulea
mambo ambayo yanakipeleka chama kubaya na wilaya hiyo.
“Mheshimiwa Waziri nipo tayari kusulubiwa katika hili,
nitasema ukweli daima ndani ya chama sitaki unafiki, hapa Mbinga kumechafuka Mkurugenzi
sasa amefikia hatua ya hata kuwahamisha waratibu elimu kata bila kufuata taratibu
kwa sababu tu ya mgogoro huu ambao anauendekeza na watu wake anaowajua yeye,
“Sisi kama chama tukiona kuna mtendaji wa serikali ana dalili
tosha ya kutaka kukiharibu chama kama ilivyo kwa mgogoro huu, hatutakuwa na
msamaha naye haki ya mtu haipotei ila inacheleweshwa,
“Kutunishiana misuli hakutakiwi, kwa wale watendaji wanaotupuuza
tusimame kidete kama viongozi wa chama kupinga jambo hili kwa nguvu kubwa”, alisema
Mbunda.
Aliongeza kuwa watendaji wa serikali wasipokuwa na
ushirikiano kati ya chama tawala kilichopo madarakani maendeleo kwa wananchi
hayatakuwepo, ni vyema viongozi wa namna hiyo wakawajibishwa mapema kwa manufaa
ya umma ili wasilipeleke taifa kubaya kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Waziri wa ulinzi na
Jeshi la kujenga Taifa anena:
Akijibu hoja juu ya mgogoro huo uliopo kati ya Mkurugenzi
mtendaji na Afisa elimu wa wilaya ya Mbinga, Waziri Mwinyi alisikitishwa na
kitendo hicho na kusema haki itendeke asionewe mtu na kama viongozi katika ngazi
ya wilaya na mkoa watashindwa kulimaliza jambo hili, ameagiza liletwe ngazi ya
taifa na yupo tayari kulifanyia kazi.
Mwinyi alisema anashangazwa na viongozi wa wilaya hiyo
kushindwa kumaliza mgogoro huo kwa wakati badala yake unaendelea kudumu kwa
muda mrefu, hadi unafikia hatua ya kuwachukiza wananchi wa Mbinga na
kuhatarisha sekta ya elimu msingi kurudi nyuma wilayani humo, wakati wilaya
hiyo hivi sasa inang’ara kitaifa kufanya vizuri katika elimu.
No comments:
Post a Comment