Sunday, November 2, 2014

OPEN DOORS YAPONGEZWA KWA KUTOA MSAADA WA PIKIPIKI TUNDURU



Na Steven Augustino,
Tunduru.

UMOJA wa makanisa wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, umelipongeza shirika  lisilokuwa la serikali la Open Doors  kwa kufanikisha upatikanaji wa msaada wa pikipiki tano zenye thamani ya shilingi milioni 10 zilizoletwa wilayani humo, kwa ajili ya kuwagawia wachungaji wa makanisa ya kikristo.

Lengo la utoaji wa pikipiki hizo ni sehemu ya msaada wa kuwezesha madhehebu hayo yaweze kutoa huduma za kichungaji kwa waumini wao. 

Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa umoja wa makanisa hayo, Mchungaji Mathias Nkoma wa Kanisa la Anglikana mjini hapa, alipokuwa akizungumza katika hafla fupi ya ugawaji wa pikipiki hizo kwa wachungaji wa makanisa hayo iliyofanyika uwanja wa kanisa la Bibilia mjini hapa.


Kwa mujibu wa Mchungaji Nkoma alisema, mpango huo uliibuliwa na shirika hilo na kuwahusisha kwa ahadi za kuwaletea Pikipiki hizo baadhi ya wachungaji wa Makanisa hayo.

Mchungaji Nkoma aliendelea kufafanua kuwa kufuatia hali hiyo mpango huo ulipata wakati mgumu hata ulipotambulishwa kwa waumini, hasa walipotakiwa kutoa kiasi kidogo cha fedha za michango kwa ajili ya kufanikisha upatikanaji wa pikipiki hizo.

Alisema kufika kwa pikipiki hizo na kugawiwa kwa wachungaji wa makanisa hayo, kutawafanya viongozi wa dini za kikisto wilayani Tunduru, kuweza kutoa huduma za kiroho hadi katika maeneo ya vijijini.

No comments: