Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
JESHI la Polisi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, limeingia
katika kashfa mpya kufuatia askari wake wa usalama barabarani kumjeruhi
mwendesha pikipiki kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali kichwani, na
kumsababishia jeraha ambalo lilisababisha dereva huyo kutokwa na damu nyingi.
Tukio hilo lilitokea Oktoba 20 mwaka huu majira ya mchana, eneo
la stendi ya magari ya abiria mjini hapa, ambapo askari huyo anayejulikana kwa
jina la Msafiri Kilango, ndiye aliyefanya kitendo hicho kwa kumchoma kichwani
dereva wa pikipiki aitwaye Erick Shonga.
Kufuatia tukio hilo hali ilibadilika mjini hapa ambapo kundi
la waendesha pikipiki liliandamana kuelekea kituo kikuu cha polisi cha wilaya
hiyo, kwa lengo la kupinga kitendo alichofanyiwa mwenzao.
Walipofika kituoni hapo walieleza malalamiko yao wakisema
kuwa askari wa usalama barabarani wilayani hapa, wamekuwa na mazoea ya
kuwanyanyasa mara kwa mara waendesha pikipiki hivyo wamechoshwa na hali hiyo.
“Sisi tumechoshwa na unyanyasaji huu ambao tunafanyiwa na
hawa askari, muda mwingi wakitukamata wanatupiga faini wanachukua hela zetu
halafu stakabadhi ya malipo halali hatupewi”, alisema Thito Mhina mmoja kati ya
madereva hao wa pikipiki.
Aliyechomwa atoa
ushuhuda:
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi dereva wa pikipiki
aliyejeruhiwa Erick Shonga alisema, amepatiwa matibabu katika hospitali ya
wilaya hiyo ambapo ameshonwa nyuzi tatu kichwani katika eneo ambalo alichomwa
na kitu chenye ncha kali kichwani.
“Huyo askari amekuwa na mazoea ya kunisimamisha barabarani
hata wakati mwingine nisipokuwa na makosa na ananiambia nimpe hela, siku
ananikamata na kunijeruhi nilimwona mkononi akiwa ameshika kisu kidogo cha kukunja,
alinikamata roba ya shingo na kuniambia kwa ukali shuka kwenye pikipiki huku
akiwa amechomoa funguo ya pikipiki yangu”
“Baada ya mimi kushuka kwenye pikipiki, huku akiwa amenishika
roba alikuwa akinivuta kuelekea kituo kidogo cha polisi kilichopo pale stendi,
nikaingia ndani ya kile kituo na kuniambia piga magoti, nilipopiga magoti ndipo
nikaona ameshika hicho kisu na kunichoma nacho kichwani na damu zikaanza kutoka
kwa wingi ambapo askari mmoja niliyemtambua kwa jina moja la Seifu ndiye
aliyenichukua na kunikimbiza hospitali kwa matibabu zaidi”, alisema Erick
Shonga.
Mkuu wa wilaya anena:
Katika hatua nyingine Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga,
alipozungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, wakati waendesha pikipiki hao
wanaandamana kuelekea kituo cha polisi yeye alichukua maamuzi ya kwenda
kuzungumza nao na kuwatuliza wasiwe na jazba wakati serikali inalifanyia kazi
tatizo hilo.
“Tutakaa kikao kujadili suala hili ili tuone tunachukua
maamuzi gani, kwa sasa siwezi kuzungumzia lolote mpaka tukae tuone hali
ilikuaje lakini ninachoweza kukuambia hapa huyu dereva wa pikipiki
aliyejeruhiwa amepewa PF 3 na yupo hospitali anapatiwa matibabu”, alisema
Ngaga.
Kamanda wa Polisi
athibitisha:
Naye Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela
alipozungumza na Mtandao huu alisema askari aliyefanya kitendo hicho aliwekwa
mahabusu katika kituo kikuu cha polisi wilayani Mbinga, na kwamba limefunguliwa
jalada la uchunguzi kwa hatua zaidi juu ya tukio hilo.
“Nyandindi hapa nasubiri jalada la uchunguzi lililetwe hapa
mkoani ili tuweze kuanza kazi ya kuchunguza tukio hili, kazi hii itakapo kamilika
tutatoa taarifa kamili”, alisema Msikhela.
No comments:
Post a Comment