Kibao hiki kinaonyesha Mkandari husika aliyefanya kazi ya ujenzi wa barabara hiyo. (Picha zote na Kassian Nyandindi) |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WAKALA wa barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Ruvuma, ameshushiwa lawama nzito kwa kushindwa kusimamia kikamilifu ujenzi wa barabara kiwango cha lami katika eneo la Mbinga mjini mkoani humo, kutokana na barabara ambayo imejengwa na wakala huyo kuanza kubomoka tabaka la juu kabla ya kukabidhiwa rasmi mikononi mwa serikali.
Barabara hiyo ambayo ujenzi wake ni
wa kilometa moja, inagharimu kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni moja na kwamba utekelezaji wake upo chini ya usimamizi
wa wakala huyo.
Malalamiko hayo yalitolewa kwa
nyakati tofauti na wakazi wa mji wa Mbinga walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, walisema kuwa ni jambo la kushangaza kuona
ujenzi wa barabara hiyo baada ya magari kuruhusiwa kupita, hata kabla
haijamaliza miezi miwili tabaka la juu la lami limeanza kubomoka.
“Kwa kweli hatukutarajia kama leo barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami halafu kabla ya kukabidhiwa
rasmi mikononi mwa serikali, inabomoka na kinachofuata hapa ni kuwekwa viraka, maana
viongozi walituhakikishia barabara yetu itajengwa vizuri na kwa kiwango bora”,
walisema.
Ujenzi wa barabara hiyo ni miongoni
mwa fedha zinazotolewa na mfuko wa barabara hapa nchini, ambapo walisema huenda
kubomoka kwa barabara hiyo kunatokana na wataalamu husika kutozingatia ipasavyo
vipimo vya kimaabara na ndio maana imeanza kubomoka kabla hata haijatumika kwa
muda mrefu.
Aidha walieleza kuwa uzembe huo
uliofanywa wa kutozingatia viwango husika, ni hasara kubwa kwa serikali
kutokana na fedha nyingi zilizotumika ambazo ni kodi za wananchi kujengea
barabara hiyo, kutofanya kazi yake kama ilivyokusudiwa.
Kampuni ya FEI – MAC LTD kutoka mjini
Songea mkoani Ruvuma, ndiyo imekabidhiwa kazi ya ujenzi wa kiwango cha lami
na kwamba ujenzi wake hadi kukamilika umechukua zaidi ya miezi sita.
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo
aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwaikambo alipoulizwa kwa njia ya simu ili
aweze kutolea ufafanuzi juu ya ujenzi wa barabara hiyo alisema, “hili tatizo
ndugu yangu ni dogo sana, ni jambo la kawaida kwa barabara ya lami kufumuka au
kubanduka tabaka la juu sina cha nyongeza zaidi ya haya”.
Mtandao huu ulipomtafuta Meneja
wa Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Ruvuma, Abraham Kissimbo ili
aweze kutolea ufafanuzi juu ya malalamiko hayo alisema yeye hana nafasi ya
kuweza kuzungumzia kwa kina juu ya ujenzi wa barabara hiyo.
“Siwezi kuzungumzia lolote kwa sasa,
hapa nilipo nina kazi nyingi za kufanya siwezi kuacha kazi nilizonazo na
kuanza kukupatia wewe maelezo juu ya kwa nini barabara hii imebomoka, lakini ninachoweza
kukuambia tutafuatilia suala hili”, alisema Kissimbo.
No comments:
Post a Comment