Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.
WAKULIMA wa kahawa wilayani Mbinga mkoa wa
Ruvuma, wameitaka serikali kuendelea kuiwezesha taasisi ya utafiti wa zao hilo
hapa nchini (TaCRI) kwa lengo la kuboresha uzalishaji kwa wakulima binafsi na
waliopo katika vikundi, ili waweze kuzalisha miche ya kahawa kwa wingi.
Sambamba na hilo pia wameshauri halmshauri za
wilaya mkoani humo ambazo hujishughulisha na kilimo cha kahawa, kuongeza maeneo
ya uzalishaji kwa kufuata kanuni bora za kilimo, ikiwemo matumizi ya aina mpya
ya miche ya kahawa (vikonyo) ambayo haishambuliwi na wadudu waharibifu kwa
urahisi.
Rai hiyo ilitolewa na wakulima hao walipokuwa
wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, ambao waliwatembelea
kuona changamoto wanazokabiliana nazo na faida wanazopata baada ya TaCRI kutoa
huduma zake.
Mkulima Festo Mapunda wa kijiji cha Sepukila
wilayani Mbinga alisema, umefika wakati sasa ni muhimu kuendelea kuunga mkono
jitihada zinazofanywa na taasisi hiyo kwani yeye na wakulima wenzake baada ya
kupata elimu ya uzalishaji wa kahawa bora, wameweza kuongeza uzalishaji kutoka
robo kilo kwa mti mmoja hadi kufikia kilo mbili au zaidi.
Godbless Shao akiwa katika bustani mama, ya kuzalishia miche ya kahawa TaCRI - Ugano iliyopo wilayani Mbinga. |
“Kiuchumi tulikuwa chini sana, lakini hivi sasa
kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo cha zao hili tunaweza kupata kahawa nyingi
na yenye ubora unaokubalika ambayo tukishapeleka mnadani kwa mauzo, tunapata
fedha na maisha yetu kiuchumi yanazidi kusonga mbele tofauti na miaka ya
nyuma”, alisema Mapunda.
Naye Ernest Komba wa kijiji cha Mtama wilayani
humo ambaye pia ni mjumbe wa TaCRI, alifafanua kuwa changamoto kubwa
wanayokabiliana nayo wakulima wa wilaya ya Mbinga ni upatikanaji wa aina mpya
ya miche ya kahawa huku akiishauri serikali kuongeza nguvu kwa taasisi hiyo,
ili iendelee kutoa elimu kwa wakulima namna ya kuzalisha miche hiyo na sio
kuiachia kazi hiyo peke yake.
“TaCRI ni msaada mkubwa sana kwa sisi wakulima
katika kuendeleza zao hili la kahawa, ni vyema serikali iongeze ruzuku kwa
taasisi hii ili miche izalishwe kwa wingi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na
kijacho”, alisema Linus Komba mkulima wa kijiji cha kilimani.
Pamoja na mambo mengine Meneja wa taasisi hiyo
kituo cha Ugano Kanda ya kusini Godbless Shao, alieleza kuwa wamekuwa wakifanya
kazi katika Halmashauri 12 zilizopo kwenye mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma ambazo
huzalisha kahawa.
Shao alisema wamekuwa wakielimisha wakulima
katika mikoa hiyo juu ya uzalishaji wa miche ya vikonyo, ambapo bustani mama za
kuzalishia miche hiyo zimejengwa katika kila halmashauri ikiwa ni lengo la
kuongeza uzalishaji wa kahawa.
“Kila halmashauri zinao wajibu wa kuhakikisha
bustani hizi za kuzalishia miche ya kahawa zinatunzwa vizuri, endapo
tutazingatia hili uhaba wa upatikanaji wa miche hii utapungua”, alisema.
Kadhalika alieleza kuwa mwitiko wa wakulima
kupanda aina hiyo mpya ya kahawa ambayo haishambuliwi na wadudu kiurahisi
umekuwa mkubwa, hivyo kinachotakiwa ni kwamba wataalamu wa ugani katika
halmashauri husika kuendelea kutimiza majukumu ya kazi zao za kila siku
ipasavyo ili kuweza kuongeza kasi ya uzalishaji.
Katika hatua nyingine Meneja huyo alishukuru
jitihada zinazofanywa na Jumuiya ya nchi za watu wa ulaya (EU) katika
kuwawezesha ufadhili wa fedha za kuendesha shughuli za TaCRI kwa manufaa ya
wakulima wanaozalisha zao la kahawa na Taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment