Gaudence Kayombo, Mbunge wa Jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma. |
Mbinga.
UMOJA wa Chemba ya Wafanyabiashara Tanzania (TCCIA) tawi la Mbinga mkoa wa
Ruvuma, umepanga mikakati na kuitaka serikali iweke taratibu zake ambazo zitahakikisha
kwamba, kila jambo la ulipaji wa kodi lifanyike pale mahali ambapo bidhaa inazalishwa kwa lengo la kukuza uchumi wa eneo husika na Taifa kwa
ujumla.
Aidha kodi za makampuni yanayofanya kazi au biashara yoyote wilayani
humo, malipo yafanyike Mbinga ikiwa ni lengo la kumfanya mfanyabiashara mkubwa
na mdogo, asiweze kuumizwa kwa kutozwa kodi kubwa.
Hayo yalisemwa katika kikao cha Wafanyabiashara hao kilichoketi
ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) mjini hapa, ambapo walieleza kwamba
wafanyabiashara wa wilaya hiyo hutozwa kodi kubwa ya mapato kutokana na baadhi
ya wafanyabiashara wakubwa, ambapo walitolea mfano kwa wale ambao hujishughulisha
na ununuzi wa zao la kahawa wilayani humo, kwenda makao makuu ya kampuni zao
yaliyopo nje ya Mbinga kulipia kodi zao.
Vilevile mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Menlick
Sanga, aliongeza kuwa licha ya wilaya hiyo kuwa na mwekezaji mkubwa wa mgodi wa
makaa ya mawe Ngaka, ambayo uchimbaji
wake hufanyika katika kijiji cha Ntunduaro kata ya Rwanda wilayani humo, bado amekuwa
halipi kodi hapa wilayani na wilaya kutonufaika na chochote hivyo ni vyema
serikali ikaliangalia hilo ili malipo husika kwa mwekezaji huyo aweze kuyafanya
hapa hapa wilayani.
“Sawa tunajua sheria inasema ulipaji wa kodi kwa kampuni
yoyote inaruhusiwa kulipa makao makuu ya kampuni husika, lakini sisi kama
jumuiya ya wafanyabiashara hapa Mbinga, tunatakiwa tusimame kidete kwa kuiomba
serikali itusaidie katika hili”, alisema.
Walisema hali hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa utoroshaji wa
mapato ya wilaya, hivyo serikali ni vyema ikaridhia ulipaji wa kodi zao
ukafanywa hapa Mbinga kwa lengo la kuongeza hata mapato ya ndani na taifa kwa
ujumla ili baadaye wafanyabiashara hao waweze kuondokana na adha wanayoipata
sasa ya kutozwa kodi kubwa ya mapato.
Katika hatua nyingine walimtaka Mbunge wa Jimbo la Mbinga,
Gaudence Kayombo kufanya kikao na wafanyabiashara wa wilaya hiyo, ili aweze
kukusanya maoni na kero zao.
Mjumbe mmoja katika kikao hicho aliyejitambulisha kwa jina la
Dominic Migambo alimlalamikia Mbunge huyo akisema, inamshangaza kuona tokea
Kayombo achaguliwe na kuingia madarakani kuliongoza Jimbo hilo, hajawahi
kufanya kikao na wafanyabiashara wa wilaya ya Mbinga jambo ambalo alihoji kero
au matatizo yao atawezaje kuyafahamu na kuyafikisha Bungeni, ili yaweze
kufanyiwa kazi.
“Huyu Kayombo tokea aingie madarakani sisi wafanyabiashara
amekuwa hatujali hata siku moja, hajawahi kutuita pamoja na kufanya naye kikao ili aweze kujua matatizo
yetu”, alisema Migambo.
Pamoja na mambo mengine wafanyabiashara hao wilayani humo,
waliweza pia kupanga taratibu za kukuza ofisi ya umoja wao kwa kuhakikisha kila
mmoja wao anajitoa kwa moyo, katika kuchangia ada na michango mbalimbali pale
inapohitajika ili waweze kusonga mbele kwa faida ya sasa na baadaye.
No comments:
Post a Comment