Mkurugenzi mtendaji, Halmashauri wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga |
Mbinga.
HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imetoa onyo
kali kwa wamiliki wa magari ya abiria kuhakikisha kuwa vijana wanaowatumia
kupiga debe katika eneo la stendi kuu mjini hapa, kuacha kunyanyasa abiria
kwani vitendo hivyo vinawadhalilisha na kuwanyima uhuru wa kuchagua basi
walipendalo wakati wanaposafiri.
Meneja wa stendi kuu ya magari ya abiria iliyopo mjini hapa,
Dustan Mapunda alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari alisema onyo hilo
limetolewa baada ya kupokea malalamiko kuwa wapiga debe wamekuwa na kawaida ya
kuwadhalilisha na kuwasumbua abiria jambo ambalo wakati mwingine husababisha
mizigo yao kupotea.
Mapunda alisema hatua kali zitachukuliwa kwa kampuni au basi
lolote ambalo litaonekana kuleta usumbufu kwa abiria na kwamba lazima
wafanyakazi wawe na vitambulisho na orodha yao ipelekwe katika kituo kidogo cha
Polisi cha stendi.
“Vitendo hivi vinawanyima uhuru abiria wetu, kwa hiyo ni
marufuku abiria kunyang’anywa mizigo, kuvutwa, kutukanwa au kufanyiwa kitendo
chochote cha kuwasumbua”, alisema Mapunda.
Pamoja na mambo mengine akizungumzia suala la usafi katika
eneo hilo la stendi, alisisitiza kuwa kila basi liwe na chombo cha kuhifadhia
takataka huku akiwataka abiria kutotupa taka ovyo kwani kufanya hivyo kunaweza
kusababisha mlipuko wa magonjwa.
Aidha Meneja huyo alikemea vitendo vya kuuza vyakula ndani ya
eneo la stendi bila mpangilio ambapo aliwat aka mama malishe kufuata taratibu
zilizowekwa kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria.
Hata hivyo aliwataka waendesha pikipiki, maarufu kwa jina la
Yeboyebo kutoingia na pikipiki ndani ya stendi hiyo badala yake watapangiwa
eneo maalumu la kupaki pikipiki zao wakati wanasubiri abiria wa kuwabeba.
No comments:
Post a Comment