Saturday, February 9, 2013

ANUSURIKA KIFO BAADA YA KUJERUHIWA NA MAMBA

Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKAZI wa kijiji cha Muhuwesi wilayani Tunduru Ruvuma  Mustafa Kalesi(52) amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Tunduru mkoani humo baada ya kunusurika kifo na kujeruhiwa vibaya na Mamba.

Majeruhi Kalesi ambaye amelazwa katika kitanda namba 7 katika wodi namba moja akiwa hajitambui, alikumbwa hivi karibuni na mkasa huo wakati akijaribu kuoga katika mto Muhuwesi, ili aweze kurejea nyumbani kwake akitokea kutoka shambani.

Mwandishi wa habari hizi alipozungumza na mashuhuda wa tukio hilo, walisema wakati akiendelea kuoga katika mto huo, ghafla alivamiwa na mamba huyo ambaye alianza kumshambulia  na kufanikiwa kumjeruhi vibaya.



Walisema katika tukio hilo Kalesi aliumia vibaya katika mguu wake wa kulia na mikono yote, ambapo mamba huyo alimtafuna na kutoboa toboa katika viungo hivyo vya mwili wake kabla ya wasamaria wema kujitokeza ambao waliendea kumuokoa kwa kumchoma kisu mamba huyo.

Akizungumzia tukio hilo kaimu afisa wanyama pori wa wilaya ya Tunduru Peter Mtani pamoja na kukiri kuwepo kwa tukio hilo alisema kuwa tayari idara yake imepeleka askari wenye silaha ili waende kuandaa mtego ambao utafanikisha kuuawa kwa mamba huyo.

Mtanio aliendelea kueleza kuwa  mamba huyo anatakiwa kuuawa haraka iwezekanavyo  ili asiendelee kusababisha madhara kwa watu wengine, ambao huvuka ama kwenda kuoga katika mto huo.


Akizungumzia hali ya majeruhi huyo mganga wa zamu katika hospitali hiyo Dkt. Jeshi Daraja alisema kuwa kutokana na hali aliyonayo majeruhi huyo, anatakiwa kukaa chini ya maafisa tabibu kwa muda mrefu ili kuokoa maisha yake.

Katika tukio hilo majeruhi huyo aliumizwa vibaya kutokana na kutafunwa  mikono yote na mguu wa kulia, hali ambayo imeathiri utendaji kazi ipasavyo wa baadhi ya viungo vya mwili wa majeruhi huyo.

No comments: