Na
Steven Augustino,
Tunduru.
BODI
ya Korosho Tanzania imeahidi
kutaifisha korosho zote ambazo hazitanunuliwa kupitia mfumo uliohalalishwa na
serikali wa stakabadhi ghalani ikiwa ni juhudi ya kuendelea kulinda maslahi ya wakulima
wa zao hilo.
Hayo
yamebainishwa na bodi hiyo kupitia barua yake yenye kumbukumbu namba CBT/M/1/VOL
XXV/40 ya Januari 23 mwaka huu, ambayo imesambazwa katika wilaya zinazolima korosho
na kuongeza kuwa tamko hilo limetolewa kufuatia
kuwepo kwa mfumuko wa walanguzi wazao hilo
ambapo wakulima huwanyonya kupitia vipimo haramu vya Kangomba.
Barua hiyo iliyosainiwa na Teofora Nyoni kwa niaba ya Mkurugenzi mkuu wa bodi hiyo, ilibainisha kuwa ili kufanikisha zoezi hilo pia amewaomba wakuu wa wilaya, wakurugenzi, viongozi wa vyama vya ushirika vya wakulima kushirikiana na Jeshi la polisi kuwadhibiti na kuwakamata walanguzi hao.
Katika waraka huo ambao mwandishi wetu anayo nakala yake,
umewaelekeza viongozi hao kuutumia kuwashtaki wahalifu hao kupitia kifungu cha sheria namba 18 kanuni ya adhabu namba 69 ya mwaka 2009 inayoielekeza bodi hiyo kutaifisha korosho zote zinazonunuliwa na kusafirishwa isivyo halali na taratibu za nchi.
Alisema
pamoja na mamlaka hayo wanaoyopewa kuitaifisha korosho hizo kutoka kwa
walanguzi hao, pia bodi hiyo imepewa mamlaka ya kuziuza korosho hizo
katika minada pamoja na kuwachukulia hatua za kuwashitaki ama kuwatoza faini
isiyo pungua fedha za kitanzania shilingi milioni 3 walanguzi hao.
Akizungumzia
tamko hilo Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho alisema barua na maelekezo yaliyotolewa
na bodi hiyo ni msaada mkubwa kwa wakulima wa wilaya yake ya Tunduru na maeneo
mengine kunakozalishwa zao hilo, ambao kwa kiasi kikubwa wamejeruhiwa na tabia
mbaya za walanguzi hao.
Nalicho
alieleza kwamba baada ya kupokea maelekezo hayo tayari ofisi yake imeandika barua
inayokazia maelekezo ya kuwadhibiti walanguzi hao, na kuisambaza kwa maafisa tarafa
wilayani humo, watendaji kata na vijiji kuongeza juhudi za kuwadhibiti walanguzi
hao na kwamba kiongozi atakayelegalega katika shughuli hiyo sheria itafuata
mkondo wake.
No comments:
Post a Comment