Wednesday, February 13, 2013

MGOGORO WA ARDHI WAIBUKA MBINGA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.


MGOGORO umeibuka katika kata ya Utiri wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, baada ya wakazi wa kata hiyo kuilalamikia idara ya ardhi wilayani humo, kwa kutofuata taratibu za upimaji ardhi bila kushirikisha wananchi.


Malalamiko hayo waliyatoa katika mkutano wa hadhara ulioketi mpakani mwa kata ya Utiri na Mbinga mjini, ambapo wakazi hao waliishutumu idara hiyo kwa kuingia eneo la kijiji cha Mtama katika kata hiyo na kuanza kupima ardhi, kwa lengo la kupanua eneo la mamlaka ya mji wa Mbinga.


Andrew Matteso mkazi wa kijiji cha Maumba alisema kitendo hicho ni sawa na ukiukwaji wa sheria zilizowekwa na serikali, hivyo wao wanachotambua eneo la mamlaka la mji huo, mpaka wake upo kati kati ya kitongoji cha kilosa na Maumba na kwamba wataalamu wa ardhi hawapaswi kupima ardhi hiyo kwa lengo la kupanua mji huo nje ya mpaka huo.


Alisema endapo kuna taratibu za kupanua mji huo, ni vyema wananchi washirikishwe kupitia vikao maalum na kuhalalisha jambo hilo, ili kuondoa migogoro isiyo ya lazima.

Kadhalika Matteso  alieleza kwamba, eneo la kata ya utiri kumechorwa ramani ya kupanua mamlaka ya mji wa Mbinga, bila wananchi kupewa taarifa kamili na ndio maana kumekuwa na malalamiko.

“”Hii ramani iliyochorwa haijafuata misingi inayotakiwa kwa kushirikisha wananchi wa kijiji husika au huu ni usaliti ambao mnataka kuzua ugomvi, ardhi hii ni ya kwetu sisi wananchi hatuhitaji kutuburuza tunahitaji mfuate taratibu”, alisema Matteso.

Vilevile katika mkutano huo baadhi ya wananchi walipozungumza na Majira, waliliomba shirika la Haki ardhi kuingilia kati mgogoro huo ili haki zao wanazodai ziweze kupatikana kwa wakati kutokana na kutokuwa na imani na uongozi wa wilaya hiyo, ambao ulituma watalaamu wake wa ardhi kwenda kuchora ramani na kupima ardhi yao bila kufuata taratibu husika ikiwemo kushirikisha wananchi.

Mkutano huo ulikuwa ukiendeshwa na mgeni rasmi diwani wa kata ya Mbinga mjini Kelvin Mapunda, ambapo kwa upande wake aliagiza wataalamu wa wilaya hiyo wafuate taratibu, ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi juu ya upanuzi wa mji huo na kulifikisha suala hili katika vikao vya mabaraza ya kata(WDC) na madiwani.







 

No comments: