Na Steven Augustino,
Tunduru.
SERIKALI Wilayani Tunduru Ruvuma imeahidi kufuatilia, kusimamia na
kuhakikisha kuwa Baraza la ardhi na nyumba linaanzishwa wilayani humo ili kuwapunguzia
kero wananchi wake.
Kauli hiyo imetolewa na katika sherehe za maadhimisho ya siku ya sheria
Tanzania,
na mkuu wa wilaya ya Chande Nalicho wakati akizungumza na wananchi waliohudhuria
maadhimisho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya mahakama ya Wwilaya hiyo
mjini Tunduru.
Kufuatia hali hiyo Nalicho akatumia nafasi hiyo kumtaka Mkurugenzi
mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, kuangalia uwezekano wa kuingiza suala
la uanzishaji wa baraza hilo
katika bajeti zake, ili angalau kuanzisha ujenzi wa majengo yatakayotumika katika
shughuli hizo za kutafsiri sheria na kutoa haki kwa walengwa.
Aidha katika taarifa hiyo mkuu huyo wa wilaya, alisema kuwa kutokuwepo
kwa baraza hilo
tangu ianzishwe wilaya ya Tunduru, kumekuwa ni miongoni mwa vikwazo kwa
wananchi wake pindi wanapokuwa na mahitaji ya kupata haki zao za kisheria,
endapo mabaraza ya ardhi ya kata yatashindwa kuitatua migogoro hiyo.
Alisema kutokana na hali hiyo kumekuwa na tabaka la watu wa kupata
huduma hiyo na kuwaacha wananchi wenye uwezo mdogo kifedha na wasiomudu kulipa
nauli ya kati ya shilingi 20,000 na shilingi 5,000 kila wanapotakiwa kusafiri
kufuata huduma hiyo muhimu, wamekuwa wakiacha haki zao zipotee kutokana na
kukosa fedha za kuwawezesha kusafiri umbali wa kilometa 264 kutoka Tunduru hadi
makao makuu ya mkoa wa Ruvuma mjini Songea ambako ndiko iliko mahakama hiyo.
Akizungumzia kukosekana kwa mahakama hiyo hakimu mfawidhi wa mahakama
ya wilaya Tunduru Ernest Mgongolo alidhibitisha kuwepo kwa kero hiyo, na
kuongeza kuwa kukosekana kwa huduma hiyo kunawanyima haki ya msingi ya kisheria
wanaokwazwa na madhila yatokanayo na kero mbalimbali za ardhi.
Kadhalika Mgongolo alikemea vikali tabai za wananchi kuchukua sheria
mikononi kwa kuwapiga, kuwaua na kuwachoma moto watuhumiwa wa matukio
mbalimbali kuwa kwa kufanya hivyo wanakiuka uhuru wa binadamu na akawaasa
kutoa ushirikiano kwa kuwakamata na kuwapeleka katika vyombo vya sheria na
kuacha tabia ya kuchukua sheria mikononi.
No comments:
Post a Comment