Monday, May 7, 2018

WAKULIMA WASHAURIWA KUJENGA MAHUSIANO NA VIONGOZI WA SERIKALI

Wakulima wa kahawa Mbinga wakipeana mawazo namna ya kuzingatia kanuni bora za uendeshaji wa vyama vyao vya ushirika.

Na Mwandishi wetu,      
Mbinga.

VIONGOZI waliopo katika Vyama vya ushirika wa kahawa Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma, wamesisitizwa kujenga mahusiano mazuri na viongozi wa Serikali ambao wamepewa dhamana ya kusimamia maendeleo ya vyama hivyo Wilayani humo, ili kuweza kuvifanya viweze kusonga mbele kimaendeleo.

Aidha imeelezwa kuwa ushirika wa zao hilo katika maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya hiyo ulifikia hatua ya kufa, kutokana na utendaji mbaya na kutokuwepo kwa ushirikiano mzuri kati ya wakulima na viongozi hao.

Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa vyama vya ushirika katika mafunzo elekezi yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mbicu hotel uliopo mjini hapa.

Sunday, May 6, 2018

WAKULIMA WA KAHAWA RUVUMA WAISHUKIA BODI YA KAHAWA


Na Kassian Nyandindi,   
Songea.

BAADHI ya Wakulima wanaozalisha zao la kahawa katika Wilaya ya Songea, Mbinga na Nyasa Mkoani Ruvuma wameitaka Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kuwawezesha kujisajili kwenye mfumo wa utoaji wa taarifa za masoko ya dunia, ili mauzo ya kahawa yao yaendane na soko hilo.

Pia walisema kuwa ili waweze kuuza kahawa yao moja kwa moja mnadani bila kupitia kwa mtu binafsi ni muhimu waingizwe kwenye mfumo huo ili watambue soko la dunia lipoje.

Walisema hayo kwa nyakati tofauti Mkoani humo wakati walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini.

Thursday, May 3, 2018

WAKULIMA MBINGA WASHAURIWA KUWEKA AKIBA YA CHAKULA

Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye.

Na Dustan Ndunguru,       
Mbinga.

SERIKALI Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma imewataka wakulima Wilayani humo kuachana na tabia ya kuuza mazao yao yote, badala yake wajenge tabia ya kuweka akiba ya chakula ili waweze kuepukana na njaa.

Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Cosmas Nshenye alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari Ofisini kwake ambao walimtembelea kwa lengo la kupata taarifa mbalimbali za maendeleo.

Nshenye alisema kuwa Serikali Wilayani humo haitasita kuchukua hatua kali kwa wakulima wenye tabia ya kuuza mazao bila kufuata taratibu na sheria zilizowekwa, ikiwemo kuwataka kuweka akiba ya chakula ili kuwanusuru na balaa la njaa linaloweza kutokea hapo baadaye.