Mbunge wa jimbo la Mbinga Gaudence Kayombo(aliyesimama) akisisitiza jambo wakati wa kumkaribisha mtaalamu wa madini kutoka Korea, Dokta Kim (katikati) ambaye ana lengo la kupanua soko la madini kwa wachimbaji wadogo wadogo wa madini na kutangaza fursa za kimaendeleo kwa mataifa mengine wilayani Mbinga. Kushoto ni mtaalamu mwenzake aitwaye Changlee. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga
mkoani Ruvuma kupitia chuo chake cha maendeleo ya jamii (FDC) kilichopo mjini
hapa, kimeingia mkataba na mtaalamu wa madini ambaye anafahamika kwa jina la
Dokta Kim kutoka nchi ya Korea kusini, kwa ajili ya kutoa mafunzo ya wiki mbili
ya utengenezaji wa vito vya thamani.
Pia mkataba huo unalenga miaka
mitano ijayo mtaalamu huyo ataweza kujenga kiwanda cha kutengeneza vito vya
thamani wilayani humo, jambo ambalo litaweza kupanua soko la ajira kwa wananchi
wa wilaya hiyo.
Akizungumza katika hafla fupi ya
kutiliana sahihi katika ukumbi wa chuo cha maendeleo uliopo Mbinga mjini, Dokta
Kim alisema yeye ni mtu wa kwanza katika nchi hiyo ya Korea kusini ambaye
anaongoza kwa utengenezaji wa vito vya thamani, hivyo anawaomba washiriki
walioteuliwa kujiunga na mafunzo hayo kuwa makini wakati watakapo kuwa
darasani.
Dokta Kim alisema kuwa wazo hili la
kuja Mbinga na kutaka kufanya hayo ni jitihada zilizofanywa na Mbunge wa jimbo
la Mbinga Gaudence Kayombo, ambapo mafunzo hayo yataweza kuwafungua vijana wa
wilaya hiyo waweze kufanya shughuli za utengenezaji wa vito hivyo na kuweza
kuondokana na umasikini.
Washiriki wa mafunzo hayo wapo 20
kutoka katika maeneo mbalimbali wilayani humo ambako madini yanachimbwa,
wametakiwa mara baada ya kumaliza kupata ujuzi wa kutengeneza vito vya thamani
kama vile pete, bangili, heleni na hata mikufu ya kuvaa shingoni waache
ubinafsi badala yake elimu hiyo waieneze kwa wengine.
“Naomba muwe na moyo wa kupokea
mafunzo haya kwa faida ya jamii ya wanambinga, soko la vito vya thamani lipo
jambo la msingi ni kutengeneza vito vyenye ubora wa hali ya juu”, alisisitiza
Dokta Kim.
Vilevile kwa upande wake Mbunge wa
jimbo la Mbinga Gaudence Kayombo alisema lengo la kumleta mtaalamu huyo wa madini,
ni kutaka pia kupanua soko la madini kwa wachimbaji wadogo wadogo wa madini na
kutangaza fursa za kimaendeleo kwa mataifa mengine wilayani humo.
No comments:
Post a Comment