Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WASHIRIKI wa mafunzo ya kutengeneza
vito vya thamani wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameiomba serikali wilayani
humo kuendelea kuunga mkono mafunzo waliyoyapata ili yaweze kuleta faida kwa
kizazi cha sasa na kijacho.
Kauli hiyo ilitolewa kupitia risala
yao iliyosomwa na mmoja kati ya washiriki hao, Editha Komba mbele ya mgeni
rasmi Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga wakati wa kufunga mafunzo hayo ya wiki
mbili yaliyofanyika katika chuo cha maendeleo ya wananchi (FDC) kilichopo mjini
hapa.
Aidha katika risala hiyo washiriki
hao walisema wameweza kujifunza kutengeneza ukataji wa vipande vya aluminiamu
na shaba, kutengeneza mapambo mbalimbali kama vile heleni, cheni na bangili.
Walieleza kuwa wameweza kujifunza kutumia
vitu vya asili kama vile mbegu za maembe, kahawa, maboga na manyoya ya kuku
kutengeneza mapambo ya asili.
Komba aliongeza kuwa wakati wanajifunza
waliweza kupata changamoto mbalimbali ikiwemo uchache wa vifaa vya kufundishia
hivyo walimuomba mkufunzi wa mafunzo hayo Profesa Kim, kutoka nchi ya Korea
kusini kuhakikisha kwamba wakati ujao mafunzo hayo yatakapotolewa tena wilayani
Mbinga kuwepo na vifaa vya kutosheleza mahitaji halisi.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo
Ngaga, aliwataka washiriki wa mafunzo hayo huko waendako wakayaendeleze kwa
wengine ili jamii kwa ujumla iweze kunufaika nayo.
Hata hivyo alieleza kuwa serikali
itaendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na taasisi mbalimbali ikiwemo
vyuo vya ufundi nchini ambavyo hutoa mafunzo yanayolenga wahitimu kujiajiri wao
wenyewe na hivyo kusaidia jamii kuondokana na ukosefu wa ajira.
No comments:
Post a Comment