Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HOSPITALI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imepewa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya
shilingi milioni 5,530,000 kwa lengo la kusaidia utoaji wa huduma bora za
matibabu kwa wagonjwa.
Vifaa hivyo vilitolewa na Mbunge wa
jimbo la Mbinga Gaudence Kayombo wakati alipokuwa ametembelea hospitalini hapo,
kwa lengo la kujionea changamoto mbalimbali ambazo zinakwamisha utoaji wa
huduma za matibabu.
Kayombo alikabidhi vifaa vya kitengo
cha maabara ambavyo ni Darubini mbili, mashine za kupimia magonjwa ya sukari na
moyo ambapo hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu wa vifaa hivyo.
Awali Mbunge huyo alisema ni jambo la
kusikitisha kuona hospitali inashindwa kutoa huduma zake ipasavyo kutokana na
kukosekana kwa madawa au vifaa tiba, hivyo aliutaka uongozi husika kuhakikisha
unatoa taarifa zake kwa wakati serikalini ili kuweza kuondokana na matatizo
hayo.
Naye Mganga mfawidhi wa hospitali ya
wilaya ya Mbinga, Elisha Robert alieleza kuwa hivi sasa wamekuwa wakijituma
kufanya kazi kwa bidii ikiwemo kuzingatia taratibu zilizowekwa, wakihakikisha
kwamba hospitali wakati wote inakuwa na vitendea kazi na madawa ya kutosha ili
kuondoa kero mbalimbali kwa wagonjwa.
No comments:
Post a Comment