Hivi ndivyo ilivyo katika chanzo cha maji Kigonsera ambako maji yametegwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu, hali ni mbaya hatua husika zinapaswa kuchukuliwa mapema.(Picha na Gwiji la matukio Ruvuma) |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
AFYA
za wakazi wa kijiji cha Kigonsera kata ya Kigonsera wilayani Mbinga mkoa wa
Ruvuma, zipo mashakani kutokana na maji wanayotumia kwa ajili ya kuendeshea
maisha yao ya kila siku kuwa machafu na kutofaa kwa matumizi ya binadamu.
Hali
hiyo imesababisha wakazi hao kutoa tamko na kutishia kwamba siku ya ujio wa
Rais Jakaya Kikwete, katika ziara ambayo anatarajia kuifanya hivi karibuni katika
kipindi cha mwezi Mei mwaka huu mkoani humo hususani katika wilaya ya Mbinga,
wapo tayari kulala barabarani kwa lengo la kushinikiza msafara huo usimame ili
waweze kutoa kilio chao kwa kiongozi huyo wa kitaifa na kiweze kufanyiwa kazi
haraka.
Walisema
kufanya hivyo kunatokana na uongozi wa wilaya hiyo kuwa na kasi ndogo, ya
uchukuaji wa hatua za kuwahamisha watu waharibifu katika eneo ambako chanzo cha
maji kimejengwa na kugharimu mradi mzima wa maji uliosambazwa kijijini hapo
kufikia shilingi milioni 479 kwa ufadhili wa benki ya dunia.
Kauli
hiyo ilitolewa na baadhi ya viongozi wa kata ya Kigonsera kwenye mazungumzo
mafupi yaliyofanyika katika ofisi za kata hiyo, yaliyojumuisha Mwenyekiti wa
halmashauri ya wilaya ya Mbinga Allanus Ngahy na viongozi wengine wa
halmashauri ya wilaya hiyo.
Walisema
chanzo cha maji hayo kuwa machafu kinatokana na uharibifu unaofanywa katika
chanzo kikuu cha maji ambacho kimejengwa katika mlima Kigonsera uliopo katika
kijiji hicho.
Walieleza
kuwa watu wachache ambao wametakiwa kuhama wanaoishi karibu na chanzo hicho,
wamekuwa na kiburi na kufikia hatua hivi sasa wanaendesha shughuli za kilimo
cha mazao ya aina mbalimbali karibu na chanzo hicho jambo ambalo linasababisha
kuwepo na uchafuzi wa mazingira na hata kutishia kutoweka kwa uoto wa asili.
“Wananchi
tunaiomba serikali ituruhusu tuchukue hatua sisi wenyewe ya kuwahamisha wale
watu kule milimani maana viongozi wetu wa wilaya inaonesha mmeshindwa, tunasema ujio wa Rais tunajiandaa kulala barabarani ikiwa
ni ishara ya kilio cha kutaka wale watu wahame, kwa nini viongozi wetu wa wilaya
hamchukui hatua za haraka”,? walihoji.
Kwa
ujumla licha ya serikali kugharimia fedha nyingi kupitia ufadhili wa benki ya
dunia kujenga mradi huo wa maji katika kijiji hicho cha Kigonsera, hali imekuwa
tete kufuatia mradi huo chanzo cha maji yalikotegwa kuchafuliwa na kufikia
hatua kuwa na uwingi wa tope na takataka ambazo zinahatarisha usalama wa maji
hayo kuyatumia binadamu, kutokana na shughuli za kilimo zinazoendelea kufanywa
huko hadi sasa.
No comments:
Post a Comment