Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUU
wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu ameutaka
uongozi wa wilaya ya Mbinga mkoani humo, kuchukua hatua mapema ya kunusuru hali
ya chanzo cha maji kilichopo kijiji cha Kigonsera kata ya Kigonsera, ambacho
kimevamiwa na watu wachache ambao huendesha shughuli za kilimo.
Aidha
watu hao wameweka makazi karibu na chanzo hicho kwa kujenga nyumba za kuishi jambo
ambalo linahatarisha kupotea kwa uoto wa asili katika chanzo.
Mwambungu
alitoa agizo hilo alipokuwa wilayani humo katika ziara yake ya kikazi, mara
baada ya kusomewa taarifa ya maendeleo ya wilaya ambayo ilisomwa na Mkuu wa
wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga.
“Hili
jambo tusilifumbie macho, tuchukue hatua sasa kwa kuhakikisha wale watu
wanahamishwa haraka ili kuweza kunusuru usalama wa chanzo kile”, alisema.
Awali Mkuu huyo wa mkoa aliuagiza uongozi wa
wilaya hiyo kuhahakisha kwamba wanaendelea kuelimisha wakulima juu ya
uzingatiaji wa kilimo bora cha zao la kahawa, ili waweze kuzalisha kwa ubora na
hatimaye wapate bei nzuri katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Pamoja
na mambo mengine aliongeza kuwa serikali imejipanga pia namna ya kukabiliana na
ununuaji wa mahindi ya wakulima, hususani katika maeneo ambayo huzalishwa kwa
wingi.
No comments:
Post a Comment