Tuesday, March 11, 2014

TANROADS RUVUMA YAENDELEA KUNYOSHEWA KIDOLE

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.


SERIKALI mkoani Ruvuma imeombwa kuchukua hatua za haraka juu ya ujenzi wa barabara ya kutoka Mbinga mjini, kwenda hospitali ya Litembo iliyopo wilayani humo, kutokana na barabara hiyo kuwa katika hali mbaya.

Rai hiyo ilitolewa na Wananchi wa wilaya ya Mbinga mkoani humo walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, ambapo walieleza kuwa kutokana na barabara hiyo kuwa na mashimo mengi ambayo ni makubwa, magari ya abiria na yale yanayobeba wagonjwa yamekuwa yakikwama na kuleta adha kubwa kwao.

Walisema wamechoshwa na ahadi hewa ambazo zimekuwa zikitolewa mara kwa mara na viongozi wa serikali wa mkoa huo, kwamba wataifanyia matengenezo na hakuna matokeo mazuri yanayoonekana kuzaa matunda juu ya kumaliza tatizo hilo ambalo limedumu kwa miaka mingi.

"Tunachohitaji hapa waifanyie matengenezo tumechoka na kauli zao ambazo hazina utekelezaji sisi ni wananchi kama walivyo wenzetu katika maeneo mengine ambayo serikali inawapelekea huduma za msingi",
walisema.


Naye Diwani wa kata ya Litembo Altho Hyera alisema barabara hiyo ina urefu wa kilometa 26 kutoka Mbinga mjini hadi katika hospitali hiyo, ina muda mrefu haijafanyiwa matengenezo jambo ambalo limekuwa likileta kero kubwa katika jamii na kuzua malalamiko ya hapa na pale.

Alisema kuwa yeye binafsi licha ya kupeleka maombi mara kwa mara katika vikao husika na hatimaye kwa Wakala wa barabara mkoani Ruvuma(TANROADS) ambaye ndiye mmiliki wa barabara hiyo hakuna hatua
zilizochukuliwa hadi sasa.

"Jambo hili nimekuwa nikilipigia sana kelele kwa viongozi husika kwa kuwaomba waifanyie matengenezo barabara hii lakini hakuna kinachoendelea, wananchi wamekuwa wakipata shida hasa kipindi hiki cha
masika kwa wale ambao wamekuwa wakisafirisha wagonjwa wao kwenda hospitali ya Litembo kwa ajili ya matibabu", alisema Hyera.

Hata hivyo alipotafutwa Meneja wa TANROADS mkoani Ruvuma Abraham Kissimbo, ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya matengenezo ya barabara hiyo hakuweza kupatikana na simu yake ilikuwa imefungwa.

No comments: