Friday, March 7, 2014

WANAFUNZI WAJISAIDIA PORINI KUTOKANA NA SHULE KUKOSA VYOO



Na Kassian Nyandindi,

Nyasa.

SHULE ya msingi Ndingine iliyopo katika kata ya Ngumbo wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa vyoo kwa muda mrefu sasa jambo ambalo lina hatarisha usalama wa afya kwa walimu na watoto wanaosoma shuleni hapo.

Mwandishi wa habari hizi amebaini na kushuhudia pia wanafunzi wakijisaidia pori lililopo jirani na shule hiyo, huku walimu wao nao wakiomba msaada katika vyoo vya wakazi wanaoishi jirani na shule hiyo.

Huenda hatua zisipochukuliwa mapema hususani katika kipindi hiki cha masika magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu na homa zingine za matumbo, zinaweza kujitokeza na kuleta madhara makubwa kwa binadamu.

Ndingine ni shule ambayo ina jumla ya wanafunzi 306 wakiwemo wavulana   163 na wasichana 143 ambapo hata mazingira ya shule hiyo sio mazuri hivyo jitihada za makusudi zinahitajika katika kunusuru hali hiyo isiweze kuendelea.


Baadhi ya wakazi na walimu ambao nimezungumza nao kwa nyakati tofauti kwa sharti la kutotaka majina yao yatajwe, walisema tatizo hilo linasababishwa na uzembe unaofanywa na uongozi husika wa halmashauri ya wilaya ya Nyasa kutotembelea shule kwa muda mrefu na kujionea hali halisi ya matatizo yaliyopo.

“Viongozi wa wilaya yetu idara ya elimu hatuja waona hapa kutembelea shule hii, ni muda mrefu umepita na ndio maana ndugu mwandishi unaona matatizo haya yakiendelea kuwepo”, walisema.

Ofisa elimu wa wilaya hiyo Robert Hyera alipoulizwa kwa njia ya simu juu ya matatizo hayo alikiri na kusema kuwa wakati wowote anatarajia kwenda huko kwa lengo la kujionea hali halisi na kuona namna gani wanachukua hatua katika kumaliza matatizo ya shule hiyo.

“Taarifa ya matatizo ya shule hii ninayo, hivi sasa nipo safarini nitakaporudi nitakwenda huko ili kuona tunachukua hatua gani”, alisema Hyera.

Juu ya suala la idara yake kutotembelea shule ya msingi Ndingine kwa muda mrefu, alisema yeye ni mgeni amehamia hivi karibuni katika wilaya hiyo hivyo hawezi kujua huko nyuma hali ilikuwaje.



No comments: